Celta Vigo yazidisha shinikizo kwa Xabi Alonso
8 Desemba 2025
Real Madrid walipoteza dhidi ya Celta Vigo kwa mabao 2-0 katika mechi ya mzungumzo wa 16 wa La Liga baada ya kumaliza mchezo wakiwa na wachezaji tisa, hali iliyoongeza shinikizo kwa kocha Xabi Alonso.
Kadi nyekundu mbili za Fran Garcia na Alvaro Carreras zimeibua mjadala kuhusu nidhamu na umakini wa kikosi cha Madrid, jambo ambalo linaweza kuathiri mechi zijazo.
Kipigo hicho kinamaanisha Real Madrid walioko nafasi ya pili na ambao watakuwa wenyeji wa Manchester City katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya mnamo siku ya Jumatano, wako alama nne nyuma ya vinara Barcelona baada ya kushinda mechi moja pekee kati ya tano zilizopita za La Liga.
Hiyo ni mara ya kwanza baada ya miaka 19 kwa Celta Vigo kushinda ugenini Santiago Bernabéu.
Baada ya mechi hiyo, Xabi Alonso alisema, "Sote tuna hasira, ni wazi kabisa huu haukuwa mchezo tulioutaka, hayakuwa matokeo tuliyoyataka. Tunapaswa kujaribu kuufunga ukurasa huu haraka iwezekanavyo."
Ingawa Alonso anakosolewa kwa mbinu zake, Rais wa klabu hiyo Florentino Pérez bado anaonekana kumpa nafasi akiamini kocha huyo anahitaji muda zaidi kurekebisha fomu ya timu.
Kuna taarifa kwamba mabishano yaliibuka kati ya kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso, na rais wa klabu Florentino Pérez. Inadaiwa Alonso alilalamika kuhusu ukosefu wa usajili wa kiungo mbunifu, akisisitiza kuwa pengo hilo limekuwa likiathiri ubora wa kikosi chake katika mechi za La Liga na mashindano ya Ulaya.