1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg yakabiliwa na mtihani dhidi ya Bayern

Josephat Charo
8 Mei 2026

Tayari wakiwa wanapambana ili kuepuka shoka la kushushwa daraja kutoka ligi kuu ya Bundesliga, Wolfsburg Jumamosi wanawakaribisha Bayern Munich ambayo bado inakabiliwa na machungu ya kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa.

https://p.dw.com/p/5DTC4
VfL Wolfsburg wanakabiliwa na kibarua kipevu dhidi ya Bayern Munich katika juhudi za kuepuka shoka la kushuka daraja
VfL Wolfsburg wanakabiliwa na kibarua kipevu dhidi ya Bayern Munich katika juhudi za kuepuka shoka la kushuka darajaPicha: Swen Pförtner/dpa/picture alliance

Tayari wawakiwa wanapambana ili kuepuka shoka la kushushwa daraja kutoka ligi kuu ya Bundesliga, Wolfsburg Jumamosi wanawakaribisha Bayern Munich ambayo bado inakabiliwa na machungu ya kupigwa kumbo na kuondolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Champions na mabingwa watetezi Paris Saint-Germain.

Wolves, ambao wamebaki katika ligi kuu tangu kupanda daraja mwaka 1997, wako katika nafasi ya 16, nafasi ya kucheza mechi za mchujo wa kushushwa daraja.

Wolfsburg wanahitaji kuwashinda mabingwa wa Bundesliga ili kuyaweka hai matumaini yao madogo ya kuvunja pengo la pointi sita hadi eneo salama na kutoka katika timu tatu za chini.

Lakini kwa St Pauli walio katika nafasi ya pili wakipumua shingoni mwao, hata sare inaweza kusaidia.

Pauli, katika nafasi za kushushwa daraja moja kwa moja, wako na alama sawa na Wolfsburg lakini nyuma kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Baada ya kukabiliana na Bayern Munich Jumamosi, Wolfsburg watasafiri kwenda kucheza ugenini na Pauli katika mchezo wa mwisho wa msimu.

Kumaliza msimu katika nafasi ya 16 kutamaanisha watacheza mechi mbili za mchujo wa kushushwa daraja dhidi ya timu ya tatu bora katika ligi ya pili. Kwa hali ilivyo sasa, timu hiyo ni Hannover, majirani wa Wolfsburg wa jimbo la Lower Saxony ambao wanajivunia ushabiki mkubwa zaidi katika eneo hilo na mara kwa mara hujaza uwanja wao wenye viti 49,000.

Bayern wanashuka dimbani wakiwa bado na machungu ya kutolewa nje ya kombe la mabingwa Ulaya na Paris Saint Germain
Bayern wanashuka dimbani wakiwa bado na machungu ya kutolewa nje ya kombe la mabingwa Ulaya na Paris Saint GermainPicha: Michael Weber/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Ingawa vilabu vya ligi kuu vina historia ya kuwashinda wapinzani wao wa ligi ya daraja la pili katika mechi za mchujo, Wolfsburg wameshinda mechi moja tu kati ya 15 zilizopita.

Ni mteremko wa kushangaza kwa Wolves, ambao walishinda Bundesliga mwaka wa 2009 na kisha Kombe la Ujerumani miaka sita baadaye, huku Kevin De Bruyne akifanikiwa kutoa mchango mkubwa na kung'ara katika klabu hiyo.

Ikimilikiwa na kampuni kubwa ya magari ya Ujerumani Volkswagen, mapungufu ya Wolfsburg si ya kifedha. Inaripotiwa kuwa Wolfsburg inashikilia nafasi ya tano miongoni mwa vilabu vyenye bili kubwa ya mishahara mikubwa zaidi katika ligi.

Kutokuwa na utulivu nje ya uwanja kumeyadhoofisha matarajio ya klabu hiyo uwanjani msimu huu.

Akiteuliwa Machi, kocha Dieter Hecking tayari ni kocha wa tatu wa kampeni ya msimu huu, huku wakurugenzi wa michezo Sebastian Schindzielorz na Peter Christiansen pia wakiwa wametimuliwa.

Kibaya zaidi, Wolfsburg pia ina rekodi mbaya dhidi ya Bayern. Hawajaishinda Bayern tangu 2015, mfululizo wa michezo 23, na kupoteza 8-1 huko Munich mapema msimu huu.

Mtu wa kutazamwa: Albert Riera

Kocha wa Eintracht Frankfurt, Albert Riera alichukua nafasi ya ukocha miezi mitatu iliyopita lakini mechi ya Ijumaa dhidi ya Borussia Dortmund inaweza kuwa nafasi yake ya mwisho kuokoa kazi yake.

Mhispania huyo asiye wa kawaida alianza kibarua chake vizuri huko Frankfurt, akirekebisha safu ya ulinzi ya timu hiyo iliyokuwa ikivuja, lakini wameshinda mara moja tu katika michezo yao sita iliyopita huku matumaini ya Eintracht Frankfurt kufuzu kwa michuano ya Ulaya msimu ujao yakipungua.

Wiki iliyopita, Riera alivishutumu vyombo vya habari kwa kupotosha ukweli kwa upashaji habari wa sumu kuhusu ripoti ya mgogoro kati ya kocha huyo na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Jonathan Burkardt.

Jonathan Burkardt amekuwa na mchango muhimu kwa timuj yake ya Eintracht Frankfurt licha ya taarifa ya vyombo vya habari kuhusu msuguano kati yake na kocha wake Albert Riera
Jonathan Burkardt amekuwa na mchango muhimu kwa timuj yake ya Eintracht Frankfurt licha ya taarifa ya vyombo vya habari kuhusu msuguano kati yake na kocha wake Albert RieraPicha: Marcus Hirnschal/osnapix/picture alliance

Siku ya Alhamisi, mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool na Manchester City alisema "hakuwa na wasiwasi hata kidogo kuhusu mustakabali wangu: hilo si muhimu.

"Kitu pekee muhimu ni kupata pointi katika mechi mbili zijazo."

"Najua jinsi mambo yanavyofanya kazi katika taaluma hii. Ninajiambia: 'Albert, usiposhinda vya kutosha, mtu mwingine atashinda'. Hivyo ndivyo ilivyo."

Takwimu muhimu

27 - St Pauli wamefunga mabao 27 pekee msimu huu -- Harry Kane pekee ana mabao 33 kwenye ligi.

29 - Bayern wameokoa pointi 29 kutokana na kupoteza nafasi msimu huu -- pointi nyingi zaidi katika historia ya Bundesliga.

32 - Haris Tabakovic wa Borussia Moenchengladbach amefunga mabao 12 kati ya mabao 37 ya timu yake msimu huu, ambayo ni asilimia 32. Hakuna mchezaji aliyetoa mchango mkubwa kwa timu yao.