1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUingereza

Sawe wa Kenya aandika historia katika mbio za marathon

26 Aprili 2026

Sabastian Sawe wa Kenya amekuwa mtu wa kwanza duniani kukimbia mbio za marathon chini ya masaa mawili. Amevunja rekodi ya dunia ya wanaume kwa sekunde 65 wakati akishinda London Marathon katika muda wa 1:59:30.

https://p.dw.com/p/5Cqlp
Sabastian Sawe akivuka utepe nje ya Kasri la Buckingham baada ya kushinda mbio za London Marathon
Sawe aliivunja rekodi ya dunia ya wanaume wakati akishinda London Marathon kwa kutumia muda wa 1:59:30.Picha: John Walton/PA Wire/empics/picture alliance

Katika tukio kubwa la historia ya michezo, Sawe aliivunja rekodi ya dunia ya wanaume kwa sekunde 65 wakati akishinda London Marathon katika muda wa saa moja, dakika 59 sekunde 30 siku ya Jumapili.

Muda wa Sawe pia ulikuwa wa kasi zaidi kwa sekunde 10 kuliko muda usio rasmi wa 1:59:40 uliowekwa na Mkenya Eliud Kipchoge mwaka wa 2019 mjini Vienna, Austria. Sawe mwenye umri wa miaka 29, ambaye alitetea taji lake la London, aliuushukuru umati mkubwa wa watu waliojipanga katika mitaa ya mji huo mkuu wa Uingereza kumshangilia. "Kilichojiri leo si kwangu peke yangu," Sawe alisema, "bali ni kwa sisi sote leo hapa London."

Mshindi wa pili, Yomif Kejelcha wa Ethiopia, pia alimaliza chini ya masaa mawili kwa kuvuka utepe na muda wa 1:59:41 katika marathon yake ya kwanza kabisa. Jacob Kiplimo wa Uganda alivunja rekodi ya awali ya dunia — iliyowekwa na Kelvin Kiptum wa Kenya huko Chicago mwaka wa 2023 — akiipunguza kwa sekunde saba alipomaliza kwa muda wa 2:00:28.

Kulikuwa na rekodi mpya katika mbio za wanawake pia, iliyowekwa na Tigst Assefa, ambaye alitetea taji lake la London Marathon katika rekodi ya dunia ya wanawake pekee ya saa 2:15:41. Rekodi hizo mbili zilizoandikwa leo zinapaswa kuidhinishwa rasmi.