Lewis-Skelly: Bado tunakibarua kigumu
11 Mei 2026
Winga wa kushoto wa Arsenal Myles Lewis-Skelly asisitiza kuwa wanajua kuliko mtu yeyote kile wanachopaswa kufanya ili kuhakikisha wanatwaa taji lao la kwanza la Ligi Kuu ya England baada ya zaidi ya miaka 20.
The Gunners wanakaribia kujihakikishia ubingwa wa England kwa mara ya kwanza tangu 2004 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya West Ham Jumapili, ingawa wenyeji walinyimwa bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi baada ya ukaguzi mrefu wa VAR.
Ushindi huo uliwaacha Arsenal kileleni wakiwa na pengo la pointi tano dhidi ya Manchester City wanaoshika nafasi ya pili, huku zikiwa zimesalia mechi mbili — nyumbani dhidi ya Burnley waliokwisha shuka daraja na ugenini dhidi ya Crystal Palace — kabla ya kukutana na Paris Saint-Germain katika fainali ya Ligi ya Mabingwa tarehe 30 Mei.
"Tunahitaji kuendeleqa kuwa wanyenyekevu,” alisema Lewis-Skelly, kijana anayeng'ara ambaye sasa amerudi kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal baada ya kukaa nje kwa muda mrefu msimu huu.
"(Chumba cha kubadilishia nguo) kimejaa furaha, msisimko, Tuna furaha, lakini tunajua kazi haijaisha.
"Tuna ‘fainali' mbili zaidi za ligi (dhidi ya Burnley na Palace), na tunapaswa kuchukua kila mechi kama inavyokuja. Mechi inayofuata ni Burnley — halafu tunaendelea.”
Winga huyo alisema ni rahisi kwa wachezaji na mashabiki kufikiria kuhusu kile kinachoweza kutokea, lakini ni muhimu kubaki kwenye wakati uliopo. "Ni lazima tuendelee kuwa makini.”
Lewis-Skelly alikuwa na msimu mzuri wa kuibuka mwaka jana, lakini alihangaika kupata nafasi kwenye kikosi cha Mikel Arteta hadi alipopewa nafasi dhidi ya Fulham mapema mwezi huu — na tangu hapo ameanza kila mechi.
"Ilikuwa ngumu mwanzoni,” alisema.
"Lakini mimi najivunia nguvu ya kiakili. Michezo si njia moja, kuna kupanda na kushuka. Kinachokufanya uwe wewe ni jinsi unavyorejea baada ya changamoto na jinsi unavyokabiliana na wakati mgumu.
"Niliwaambia familia na marafiki, ‘Sitaki kusikia kelele za mitandaoni. Niacheni niishi wakati huu, nikabiliane na changamoto hii na nitoke upande mwingine.'”
Malalamiko ya VAR
Kipa wa West Ham, Mads Hermansen, anaamini msongamano na kusukumana kwenye kona umekuwa tatizo kubwa katika Ligi Kuu baada ya VAR kukataa bao la kusawazisha dhidi ya Arsenal kwa madai ya kumfanyia madhambi kipa David Raya.
West Ham walidhani wamepata pointi muhimu baada ya Callum Wilson kusawazisha katika dakika za majeruhi, baada ya Raya kuangusha mpira. Lakini bao hilo lilikataliwa na mwamuzi Chris Kavanagh baada ya ukaguzi mrefu na kuangalia skrini ya uwanjani, kwa kosa la Pablo dhidi ya Raya.
Uamuzi huo ulifanya bao la Leandro Trossard dakika ya 82 kuwa la ushindi, likiwaweka Arsenal kileleni kwa pengo la pointi tano na kuwaacha West Ham katika nafasi ya kushuka daraja wakiwa na mechi mbili tu.
West Ham walikasirishwa na uamuzi huo na wanaripotiwa kutaka kuwasilisha malalamiko kwa chama cha waamuzi (PGMOL).
Hermansen alisema: "Ukiuliza kipa yeyote wa ligi kama amewahi kuzuiwa, kuvutwa au kusukumwa kwenye kona msimu huu, hutapata hata mmoja ambaye hajapitia hilo.
"Kwa hiyo kutoa uamuzi huu dhidi ya West Ham, sielewi kwa nini.”
Alisema video inaonyesha kuvutwa jezi kwa Mavropanos, Soucek na hata Pablo kabla ya bao, na kuhoji kwa nini tukio hilo pekee lilichaguliwa.
Mchezaji huyo wa Denmark mwenye miaka 25 alikiri Raya alizuiwa, lakini akauliza kwa nini matukio mengine kama hayo hayajapewa adhabu msimu mzima.
"Ninakubali ni fkosa,” alisema. "Lakini kwa yale yaliyotokea msimu huu — vizuizi haramu, kuvutwa, kusukumwa kwa makipa — sielewi kwa nini hili limetolewa. Hilo tu.
"Nimezungumza na David baada ya mechi na tuna uzoefu sawa msimu huu. Bila shaka ana haki ya kudai kuchezewa vibaya, lakini unaweza kupata matukio mengi ambayo yameamuliwa tofauti.”