1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kocha Arbeloa: Ushirikiano ni lazima kwa Real Madrid

11 Mei 2026

Kocha Alvaro Arbeloa asema Real Madrid inahitaji umoja na mpango wazi baada ya kufungwa na Barcelona na kukosa taji kwa mwaka wa pili, akisisitiza kujifunza makosa na kuangalia msimu ujao.

https://p.dw.com/p/5DbG0
Kocha -Alvaro Arbeloa
Kocha Alvaro Arbeloa asema anaelewa hasira ya mashabiki wa Real Madrid baada ya timu kumaliza bila taji kubwa kwa mwaka wa pili mfululizo.Picha: Cody Froggatt/Sportimage/IMAGO

Kocha wa Real Madrid, Alvaro Arbeloa, amesema klabu yake inahitaji kufanya kazi kwa umoja zaidi kama timu badala ya kutegemea uwezo wa wachezaji mmoja mmoja, baada ya Barcelona kuwafunga na kutwaa tena taji la La Liga.

Barca waliichapa Los Blancos 2-0 katika El Clásico kwenye uwanja wa Camp Nou na kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo wakiwa wamebakiwa na mechi tatu.

Arbeloa aliwaambia waandishi wa habari:

"Tunahitaji kuchukua hatua ya pamoja, kuwa na wazo wazi zaidi kuhusu tunachotaka kufanya. Kuweka maslahi ya timu mbele ya mtu mmoja mmoja, kwa sababu zaidi ya kipaji, tunahitaji kuwa na mpango ulio wazi, na kwangu huu ndio mwanzo."

"Zaidi ya yote, tunapaswa kujifunza kwamba tumepoteza pointi nyingi dhidi ya timu na katika mechi ambazo hatukupaswa kupoteza."

Baada ya kumsajili nyota wa Ufaransa Kylian Mbappé majira ya kiangazi 2024, Madrid imekuwa ikikosa uwiano wanapocheza pamoja na Vinícius Júnior na Jude Bellingham.

Mbappé, ambaye ndiye mfungaji bora wa Madrid msimu huu, hakuweza kucheza dhidi ya Barcelona kutokana na jeraha la paja. Nahodha huyo wa Ufaransa alikosolewa baada ya kwenda likizo Sardinia wakati wa kipindi chake cha kupona.

"Ningependa awe asilimia mia moja na aweze kucheza, hicho ndicho ningependa." Arbeloa alisema.

Kocha huyo alisema anaelewa mashabiki kuwa na hasira msimu huu baada ya timu kumaliza bila taji kubwa kwa mwaka wa pili mfululizo.

"Hatuwezi kuwaambia mashabiki mengi, kwa sababu tunaelewa hasira yao, kutoridhika kwao, jinsi wanavyoweza kuwa na msimu huu," alisema.

"Tunachoweza kufanya ni kufanya kazi, tukitazama mbele, tukijifunza kutokana na makosa ya mwaka huu, tukijua kwamba Real Madrid daima hurudi."

Inasemekana Arbeloa huenda asiendelee kuwa kocha msimu ujao, huku kocha wa zamani wa Madrid José Mourinho akihusishwa na kurejea.

Arbeloa alimalizia kwa kusema: "Tutakuwa na mazungumzo na klabu, kama ilivyo kawaida, na ninachotaka kwa sasa ni timu kumaliza msimu vizuri. Hilo ndilo lengo langu… na kuhusu baadaye tutaona kuanzia tarehe 24 au 25 Mei."