Bobi Wine asema mkewe ameshambuliwa na wanajeshi
24 Januari 2026
Wine amesema kwenye ujumbe kupitia ukurasa wake wa X kwamba "mamia ya wanajeshi" waliivamia nyumbani wakati hayupo, wakapora vitu na kumshambulia mkewe.
"Walimzuia mke wangu chini ya mtutu wa bunduki, wakimtaka asema mahala nilipo," ameandika kwenye ujumbe huo. "Walimkaba na kumshambulia".
"Mke wangu amekimbizwa hospitali na hadi sasa bado amelazwa -- akipitia mateso ya majereha ya mwili na ya kisaikolojia", umeelendelea kusema ujumbe huo wa Wine.
Wine yuko mafichoni tangu baada ya uchaguzi mkuu wa Uganda wa Januari 15 ambao Rais Yoweri Museveni, 81, alichaguliwa tena kwa muhula wa saba -- matokeo ambayo kiongozi huyo wa upinzani ameyaita "wizi wa mchana kweupe".
Museveni alishinda uchaguzi wa katikati ya Januari kwa asilimia 71.65 ya kura ikilinganishwa na asilimia 24.72 alizopata Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, mwanamuziki aliyegeukia siasa.
Mkuu wa jeshi Uganda ajitapa kuhujumu upinzani
Wafuatiliaji wa hali ya mambo nchini Uganda pamoja na mashirika ya kiraia waliyakosoa matokeo hayo, wakitaja matukio mfano wa kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kwa siku kadhaa na ukandamizaji dhidi ya upinzani kuwa doa kwa mchakato huo wa kidemokrasia.
Mtoto wa kiume wa rais Museveni ambaye pia ni mkuu wa majeshi ya Uganda, Muhoozi Kainerugaba, alitoa vitisho kwenye mtandao wa X vya kumsaka na kumuua Wine, katika ujumbe ambao hivi sasa umefutwa.
Kainerugaba pia alijitapa siku ya Ijumaa kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba "tayari tumewaua magaidi 30 wa NUP", akizungumzia chama cha Bobi Wine cha National Unity Platform.
"Tumewakamata zaidi ya wahuni 2,000 ambao Kabobi alitumai angewatumia," aliongeza Kainerugaba, akitumia jina la dhihaka alilompachika Wine.
Wakili wa Bobi Wine ataka usalama wa mteja wake uhakikishwe kimataifa
Kufuatia vitisho hivyo, mwanasheria wa Bobi Wine ameutolea mwito Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kutafuta hakikisho kwa usalama wa Wine ambao umetetereka tangu baada ya uchaguzi uliogubikwa na
"Chini ya kiwingu cha matamshi ya ovyo, tunairai jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa, kushinikiza kutolewe hakikisho la haraka na linalopima la usalama na kuhakikisha (Wine) anaweza kurudi nyumba kwa familia yake bila madhara," amesema Robert Amsterdam, mwanasheria wa mwanasiasa huyo wa upinzani.
"Bw. Wine hajafanya kosa lolote. Tatizo lake pekee ni kufichua, kwa mara nyingine, ukatili na uhalisia wa utawala wa kidikteta wa Rais Museveni, kupitia upinzani wa amani na kutimiza haki zake za msingi," ameongeza mwanasheria huyo.
Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi wake mkubwa, ukisema: "Tunasikitika na ghasia pamoja na vitisho vya kabla na baada ya uchaguzi, hususani vinavyoelekezwa kwa kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anafuatilia "kwa wasiwasi hali ya kisiasa nchini Uganda baada ya uchaguzi, ikiwemo taarifa za kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kushambuliwa kwa viongozi na wafuasi wa upinzani".