1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Trump kufanya ziara kinzani mpaka wa Marekani-Mexico

Bruce Amani
29 Februari 2024

Rais wa Marekani Joe Biden na mpinzani wake Donald Trump wanafanya ziara leo kwenye mpaka wa Marekani na Mexico kuelekea uchaguzi wa rais Novemba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4d2UI
Mpaka kati ya Marekani na Mexico
Uhamiaji hasa kupitia mpaka wa Marekani na Mexico ni suala muhimu katika uchaguzi wa Marekani mwaka huu.Picha: GUILLERMO ARIAS/AFP/Getty Images

Rais wa Marekani Joe Biden na mpinzani wake Donald Trump wanafanya ziara leo kwenye mpaka wa Marekani na Mexico katika jitihada za kuwashawishi wapiga kura kuhusu mojawapo ya masuala tete zaidi katika uchaguzi wa rais unaopangwa Novemba.

Ziara hizo za jimboni Texas zinajiri wakati ambapo idadi kubwa ya wahamiaji wanaoingia Marekani inasababisha kitisho kikubwa kwa nafasi za Biden za kumuzuia Trump kurejea Ikulu ya White House.

Uchaguzi wa Marekani | Donald Trump na Joe Biden
Rais Joe Biden huenda akachuana na hasimu wake wa 2020 Donald Trump, katika uchaguzi wa mwaka huu.Picha: Jeff Chiu/AP Photo/picture alliance

Mdemocrat Biden atakutana na maafisa wa ulinzi wa mpakani na wengine wa usalama katika mji wa Brownsville, Texas, wakati Mrepublican akielekea eneo la Eagle Pass, karibu kilometa 300 katika upande wa magharibi.

Soma pia:Biden atangazwa kuwa katika hali nzuri kutekeleza majukumu yake 

Biden amekuwa akipambana kusuluhisha suala la mpakani lenye madhara makubwa kisiasa kwa kuwalaumu WaRepublican katika bunge la Congress kwa kushindwa kuyaunga mkono mageuzi ya uhamiaji yaliyojadiliwa kwa miezi kadhaa na pande zote mbili za uwakilishi bungeni.

Trump anadai kuwa wahamiaji wanawauwa watu wa Marekani.