Baraza la usalama latilia mashaka amani ya Kongo | Matukio ya Afrika | DW | 25.02.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Baraza la usalama latilia mashaka amani ya Kongo

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema bado lina wasiwasi mkubwa juu ya hali inayozidi kuwa mbaya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, licha ya kusainiwa kwa mkataba mpya wa amani siku ya Jumapili.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Joseph Kabila.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Joseph Kabila.

Baraza hilo lenye wanachama 15 ambao kwa sasa wanahusisha pia Rwanda lililaani tena kundi la waasi wa M23, ambalo liliteka maeneo mashariki mwa Kongo, na ni moja ya shabaha muhimu za makubaliano ya Umoja wa Mataifa yaliyosainiwa Jumapili ya tarehe 24.02.2013 na mataifa 11 mjini Addis Ababa.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akiwasili katika makao makuu ya Umoja wa Afrika kushiriki zoezi za utiaji saini makubaliano hayo.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akiwasili katika makao makuu ya Umoja wa Afrika kushiriki zoezi za utiaji saini makubaliano hayo.

Hali bado si shwari

Rwanda na Uganda, ambazo pia zilisaini makubaliano hayo mapya, zilituhumiwa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwa kuliunga mkono kundi la M23, ambalo lilianzisha uasi dhidi ya serikali ya Jamhurui ya Kidemokrasi ya Kongo mwaka uliyopita. Baraza la usalama lilikaribisha makubaliano hayo mapya yaliyoratibiwa na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon, lakini wajumbe wake walisema bado wana wasiwasi juu ya hali ya usalama na ya kibinaadamu inayozidi kudorora katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo ilirejelea matakwa yake kwa M23 kuacha mara moja majaribio yake ya kuanzisha utawala mwingine kinyume na sheria. Baraza pia liliyataka makundi ya M23, lile la kabila ya Kihutu la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) na makundi mengine yenye silaha kuachana na shughuli zozote zinazovuruga utulivu. Mkuu wa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Roger Meece, alionya siku ya Ijumaa kuwa mgogoro mkubwa unaweza kuibuka muda wowote.

Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Afrika Kusini, Msumbiji, Rwanda, Tanzania, Uganda, Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Zambia zilisaini makubaliano ya jijini Addis Ababa yanayozitaka nchi za kanda ya maziwa makuu kujizuia kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Makubaliano hayo pia yanalenga kuzifanyia mageuzi, taasisi dhaifu za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na yanaweza kupelekea kuanzishwa kwa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa kuingilia kati mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na pia kuunda nafasi ya Mjumbe Maalum kwa ajli ya Kanda ya maziwa Makuu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akihutubia washiriki wa mkutano wa utiaji saini makubaliano hayo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akihutubia washiriki wa mkutano wa utiaji saini makubaliano hayo.

Matumaini ya enzi mpya

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon alielezea matumaini ya kuanzishwa kwa enzi mpya ya amani nchini Kongo na kanda ya Maziwa makuu kwa ujumla, na kuongeza kuwa atateua mjumbe Maalum kwa ajili ya kanda hiyo mapema."Kusainiwa kwa makubaliano hayo ni tukio muhimu, lakini ni hatua ya mwanzo tu ya utaratibu mpana ambao utahitaji ushiriki endelevu wa wadau wote," alisema Ban.

Viongozi wa Afrika walishindwa kusaini makubaliano hayo mwezi uliyopita, baada ya kushindwa kukubaliana juu ya nani atakaeongoza kikosi maalum kilichokuwa kimependekezwa. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Suzan Rice, alikaribisha makubaliano hayo na kuwataka majirani wa Kongo kuheshimu uhuru wa nchi hiyo na mipaka yake, katika matamshi ambayo yalizilenga Uganda na Rwanda bila kutaja majina.

Uasi mpya uliyoanzishwa na kundi la M23 Mei mwaka 2012 umesababisha mapigano zaidi na kuwalaazimisha raia wengi kuyakimbia makaazi yao. Mwezi Novemba waasi hao waliuteka kwa muda mji wa Goma,lakini waliuachia ili kuanzisha mazungumzo ya amani, ambayo yanaendelea mjini Kampala nchini Uganda.

Waasi wa M23, moja ya makundi yaliyolengwa na makubaliano ya Addis Ababa, walipojiondoa kutoka mji wa Goma Desemba 1 mwaka jana, ili kupisha mazungumzo ya Kampala.

Waasi wa M23, moja ya makundi yaliyolengwa na makubaliano ya Addis Ababa, walipojiondoa kutoka mji wa Goma Desemba 1 mwaka jana, ili kupisha mazungumzo ya Kampala.

Madai ya waasi

Mazungumzo hayo tofauti kati ya serikali ya Kongo na waasi yanalenga kufikia makubaliano juu ya masuala kadhaa ya kiuchumi, kisiasa na usalama, ikiwemo kutoa msamaha kwa makosa ya kivita na uasi, kuachiwa wafungwa wa kisiasa na fidia ya uharibifu kutokana na vita.

Lakini waasi wamepanua madai yao na kuongeza kuondolewa kwa rais Joseph Kabila, na kukombolewa kwa Kongo nzima. Bertrand Bisimwa, msemaji wa M23 alisema hajasoma makubaliano ya Addis Ababa kikamilifu, lakini akesema anatumaini hayatachochea upya mapigano kati yao na wanajeshi wa serikali.

"Nichachoweza kusema ni kwamba kama wanachagua njia ya amani sisi tuko sawa na hilo,lakini kama wanchagua kuendelea na vita basi tunapinga hilo," aliliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters. Makamu wa rais wa Uganda Edward Kiwanuka Sekandi alisema mazungumzo ya mjini Kampala sasa yamejikita katika suala la usalama, na kwamba majadiliano yanaonyesha matunda.

Rais Joseph Kabila alisema mazungumzona waasi yataendelea, lakini aliongeza kuwa muda uliyobakia ni mdogo kabla ya tarehe ya mwisho ya kuyakamilisha ambayo ni Machi 15. "Tulichokifanya mjini Addis Ababa ni hatua tu ya kidiplomasia. Majadiliano ya mjini Kampala yataendelea lakini tunahitaji kuzingatia ukweli kwamba hatuna muda wa kutosha," Kabila aliuambia mkutano wa waandishi wa habari baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya Addis Ababa.

Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema makubaliano ya Addis siyo mwisho wa mchakato wa amani.

Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema makubaliano ya Addis siyo mwisho wa mchakato wa amani.

Makubaliano ya Addis siyo mwisho

Migogoro ya kufuatana inayovuka mipaka imeua na kuhamisha mamilioni katika bonde la mto Kongo tangu enzi za ukoloni, ikichochewa kwa kiasi kikubwa na migawanyiko ya kisiasa na kikabila, na ushindani wa kudhibiti maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini kama dhahabu, bati, Wolframi na Coltan, madini yenye thamani kubwa yanayotumiwa katika utengenezaji wa simu za mkononi.

Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema makubaliano ya Jumapili yasichukuliwe kama ndiyo mwisho wa mambo yote, lakini kama sehemu ya mchakato wa amani unaoendelea. "Wakati tunaendelea na juhudi zetu, tunapaswa kukumbuka, haki, maslahi na matarajio ya wakaazi wanaoathirika na vurugu zinazoendelea," alisema.

Lakini Mchambuzi wa masuala ya kanda ya maziwa makuu na muandishi wa kitabu cha "Congo Masquerade" Theodore Trefon, alisema anaamini makubaliano ya Addis Ababa, na mazungumzo ya amani yaliyokwama mjini Kampala yalishindwa kuja na suluhisho la kudumu au kushughulikia malamiko ya msingi ambayo yanachochea vurugu katika kanda hiyo.

"Huwezi kulaazimisha amani kutoka juu au nje kwa watu wasiotaka amani. Wahusika wengi ndani ya Kongo wana agenda zilizojificha," Trefon aliiambia Reuters kutoka mjini Brussels.

Kwa upande mwingine kundi la waasi la M23 limeyapokeaje makubaliano hayo. Swali ambalo Sekione Kitojo alumuuliza msemaji wa kundi hilo la M23 Bertrand Bisimwa ambaye yuko mjini Kampala hivi sasa. Kusikiliza mahojiano haya bonyeza alama ya kusikiliza masikioni hapo chini.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, rtre.
Mhariri: Daniel Gakuba

DW inapendekeza

Sauti na Vidio Kuhusu Mada