1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mmtendaji mwingine wa utawala wa Trump atimuliwa

Iddi Ssessanga
30 Septemba 2017

Waziri wa afya wa Marekani Tom Price alikumbwa na kashfa baada ya kufichuliwa kuwa alitumia fedha nyingi za umma kukodi ndege binafsi. Ikulu ya White House imetangaza punguzo kubwa katika matumizi binafsi kwa mawaziri.

https://p.dw.com/p/2l0Of
USA Washington Präsident Trump nach der zurückgezogenen Gesundheitsreform
Picha: Reuters/C. Barria

Waziri wa afya na huduma za kibinadamu wa Marekani Tom Price amejiuzlu kufuatia ukosoaji mkubwa juu ya matumizi yake ya ndege binafsi za kukodi kwa safari za kiserikali. Price alitumia ndege za bei ghali katika matukio 26 tofauti na kuwagharimu walipakodi kiasi cha dola 400,000, kwa mujibu wa shirika la habari la Politico. Alijaribu kufunika kashifa hiyo kwa kurudisha sehemu ya fedha hizo.

Rais wa Marekani Donald Trump alionya siku ya Ijumaa kuwa alikuwa anatafakari kuhusu mustakabali wa Price. "Sipendi madanganyo ya macho," Trump aliwaambia awali waandishi wa habari, kwa sababu rais huyo alikuwa anajaribu kuokoa fedha za walipa kodi. " Sijafurahishwa, Naweza kuwaambia sijafurahishwa," alisema.

Safari hizo zilielezwa kuwa za kiserikali, lakini zilihusisha vituo ambako Price anamiliki mali. Kashfa hiyo ilichochea uchunguzi mpana kuhusu gharama za usafiri za wateule wa juu wa kisiasa. Kujiuzlu kwa Price kunamfanya kuwa karibuni zaidi katika msururu wa maafisa walioondoka katika utawala wa Trump - baadhi wakilazimishwa na baadhi kwa hiari.

Tom Price
Tom Price, aliekuwa waziri wa afya na huduma za kibinadamu katika utawala wa Trump ameachia ngazi baada ya kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za umma.Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Kashfa yapelekea mabadiliko ya sera

Baadae Ijumaa White House ilisema kwamba inampa mkuu wa shughuli za ikulu John Kelly, mamlaka ya kuidhinisha safari za kiserikali - kwenye ndege zinazomilikiwa na serikali na za kukodi. Mkurugenzi wa bajeti wa White House Mick Mulvaney alitoa miongozo mipya, na kuwafahamisha wakuu wa idara za mhimili wa utawala kwamba wao ni watumishi wa umma na kwamba kila senti wanayoitumia inatoka kwa walipakodi.

Mulvaney pia aliwaambia wakuu wa idara na mawaziri kuzingatia matumizi zaidi ya ndege za abiria kama njia bora zaidi ya matumizi ya fedha za umma, hata kwa ziara za maafisa wa juu waandamizi isipokuwa kwa wachache tu.

Msimamizi wa wakala wa ulinzi wa mazingira Scott Pruitt, waziri wa fedha Steven Mnuchin, na waziri wa mambo ya ndani Ryan Zinke, pia wamemulikwa kutokana na gharama zao za usafiri. Wakosoaji wamemshambulia Zinke kwa matumizi yake ya ndege za kukodi tangu alipoingia ofisini mwezi Machi, ikiwemo safari ya usiku wa manane kutoka Las Vegas kwenda nyumbani kwake jimboni Montana, iliogharimu dola 12,375. Alipinga ukosoaji huo akiutaja kama "upuuzi  kuhusu usafiri."

Mwezi Agosti waziri wa fedha Mnuschin - tajiri na mbia wa zamani wa benki wa Wall Street, alishinikizwa kufafanua matumizi ya ndege ya serikali kwenda kwa mke wake jimboni Kentucky. Safari hiyo ilielezwa kama ziara ya hifadhi ya dhahabu ya Marekani huko Fort Knox, Kentucky, lakini ambayo wakosoaji wanadai ililenga hasa kuangalia kupatwa kwa jua.

Mnuchin aliomba radhi baada ya mke wake, Louise Linton, kuweka picha kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, ikimuonyesha akishuka kwenye ndege akiwa amebeba nguo za kimtindo na vifaa vingine.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape, rtre, afpe.

Mhariri: John Juma