ANC yaendelea kumshinikiza rais Zuma ajiuzulu | Matukio ya Afrika | DW | 09.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

ANC yaendelea kumshinikiza rais Zuma ajiuzulu

Kiongozi wa chama tawala Afrika Kusini ANC, Cyril Ramaphosa amejiondoa katika matukio ya umma ili kushughulikia mambo muhimu. Ramaphosa amekuwa katika hatua za mwisho za kumlazimisha Jacob Zuma kuachia ngazi

Zuma ambaye amekuwa madarakani kuanzia mwaka 2009 anayeandamwa kwa kashfa za ufisadi, amekuwa akiishi bila ya kujua hatma yake baada ya Ramaphosa kuchukua nafasi yake kama kiongozi wa chama tawala cha ANC mwezi Desemba mwaka jana.

Ramaphosa na wanachama sita wa juu katika chama hicho walio na nguvu walipaswa kumtembelea Askofu Mkuu wa Afrika Kusini aliyestaafu, Desmond Tutu pamoja na wafuasi wa chama hicho katika matukio mbalimbali mjini Cape Town, lakini kulingana na msemaji wa ANC shughuli hizo hazitafanyika kufuatia viongozi hao kuwa na mambo mengine muhimu ya kufanya.

Afisa mwengine wa ANC amesema kubadilika kwa ratiba ya viongozi inatokana na msukumo kutoka kwa chama hicho, kumtaka Zuma ajiuzulu. "Sote tunajua na kutazamia kwamba, wanashughulikia jambo linaloikumba nchi yetu kwa sasa," alisema Faiez Jacobs Katibu wa Mkoa wa chama hicho tawala Afrika Kusini alipokuwa akizungumza na televisheni ya eNCA.

Ramaphosa amekuwa akimshinikiza Zuma ajiuzulu, na awali alisema ana matumaini ya kumaliza mazungumzo yake na Zuma yaliyoanza siku ya Jumanne ya namna ya kubadilishana madaraka katika siku zijazo. Alisema haya yote yanafanyika kwa maslahi ya nchi. Hata hivyo, msemaji wa Rais Jacob Zuma hakuweza kupatikana ili kutoa maoni yake juu ya sakata hilo.

Südafrika Präsident Jacob Zuma & Vize-Präsident Cyril Ramaphosa (Reuters/S. Sibeko)

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na makamu wa rais Cyril Ramaphosa

Kiongozi wa ANC, Cyril Ramaphosa anatarajiwa kutoa hotuba yake siku ya Jumapili kama sehemu ya sherehe zitakazosalia mwaka mzima za kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa shujaa wa ukombozi aliyekuwa baba wa Taifa la Afrika Kusini Nelson Mandela. Kwa upande wake Zuma alitarajiwa kuzindua sherehe za kutoa tuzo za kidiplomasia mjini Cape Town siku ya Jumamosi, lakini sherehe hiyo imeahirishwa.

Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 75 amekuwa rais wa Afrika Kusini aliye na utata tangu kumalizika kwa utawala wa wazungu mwaka 1994, kwa miaka tisa ya uongozi wake uchumi wa taifa hilo umeshuka, ukosefu wa ajira umeongezeka huku yeye mwenyewe akiandamwa na kashfa mbalimbali za ufisadi.

Anakabiliwa na keshi mahakamani ikiwemo hatua inayohusiana na malipo 783 anayodaiwa kupokea yanayohusishswa na mpango wa silaha kabla ya kuingia madarakani mwaka 2009. Aidha chama tawala cha ANC kimekuwa na shinikizo kutoka ndani ya chama na umma kumuondoa Zuma madarakani.

Wakati huo huo, wachambuzi wa kisiasa wanasema chama hicho kimesukumwa na kutakiwa kuchukua uamuzi wa haraka. Mmoja wa wachambuzi hao Ralph Mathekga ameliambia shirika la habari la AFP kwamba anadhani huenda chama hicho kikatangaza kitu mwishoni mwa juma hili.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP/AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo