1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyeendesha kesi dhidi ya washirika wa Trump ajiuzulu

20 Juni 2020

Mwanasheria aliyesimamia mashitaka dhidi ya washirika wa karibu wa Rais Donald Trump wa Marekani, na uchunguzi dhidi ya wakili wake binafsi, Rudy Giulaini, anaondoka kwenye wadhifa wake. 

https://p.dw.com/p/3e4OL
US-Anwalt Geoffrey Berman
Picha: Reuters/NBC

Taarifa iliyotolewa jana na Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr, inasema kuwa Geoffrey Berman, anajiuzulu nafasi yake kama mwanasheria mkuu wa New York, na kwamba Trump amedhamiria kumteua mtu mwengine kuchukuwa nafasi hiyo, kuanzia tarehe 3 Julai. 

Hakukutajwa sababu za Berman kujiuzulu ikiwa ni zaidi ya miaka miwili tangu ashikilie nafasi hiyo, lakini tangazo hilo lilitolewa, baada ya Mwanasheria Mkuu Barr kukutana na maafisa wa polisi ya New York.

Kwa mujibu wa Barr, Trump atamteuwa mwenyekiti wa sasa wa kamisheni ya usalama, Jay Clayton, kushikilia nafasi ya Berman, ingawa wadadisi wanasema mwanasheria huyo hana uzoefu wowote wa ofisi ya mwendesha mashitaka wa serikali kuu. 

Kabla ya kushikilia wadhifa wake wa sasa, Clayton alikuwa mwanasheria wa Wall Street mwenye mafanikio, akiwa ameziwakilisha na kuzishauri kampuni kadhaa kama vile Goldman Sacks, Barclays, Deutsche Bank na UBS. 

Akiwa mwenyekiti wa kamisheni ya usalama na hisa, Clayton amesimamia shinikizo la kulegeza kanuni zinazoathiri Wall Street na masoko ya fedha, kama alivyoahidi Trump alipoingia madarakani.

Mashaka ya kutenguliwa

USA | William Barr
Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr.Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/S. Walsh

Barr alimpa Berman nafasi nyengine kwenye wizara ya sheria, ikiwemo ya kuendesha kitengo cha kesi za hukukia, lakini mwanasheria huyo alikataa, kwa mujibu wa chanzo kimoja ndani ya wizara ya sheria. 

Kuondoka kwa Berman kunakuja siku chache baada ya tuhuma za mshauri wa zamani wa masuala ya usalama wa Rais Trump, John Bolton, kwamba rais huyo alijaribu kuingilia uchunguzi uliokuwa ukifanywa na Berman juu ya Benki ya Halk ya Uturuki, katika jitihada za kusaka makubaliano na Rais Tayyip Erdogan.

Hapana shaka, kuondoka kwa Berman kunazidi kuongea maswali kutoka kwa wajumbe wa chama cha Democrat dhidi ya Barr, ambaye wanamshutumu kujigeuza kuwa mwanasheria binafsi wa Rais Trump, badala ya kuwa mwanasheria wa Marekani.

Aliyewahi kushikilia wadhifa wa mwanasheria mkuu wa Marekani, Preet Bharara, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba hafikirii kwamba Berman amejiuzulu mwenyewe. 

"Kwa nini rais anamfukuza mwanasheria mkuu aliyemteuwa mwenyewe usiku wa Ijumaa ikiwa ni miezi mitano tu kabla ya uchaguzi?" Alihoji mwanasheria huyo.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: