Alabama: Roy Moore ashindwa na Doug Jones | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Alabama: Roy Moore ashindwa na Doug Jones

Mwanasiasa wa chama cha Democratic nchini Marekani Doug Jones, ameshinda katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha Useneta katika jimbo la Alabama, hili likiwa ni pigo kubwa kwa rais wa Marekani Donald Trump.

Ushindi wa chama cha democrat katika jimbo hilo la Alabama, ni tetemeko kubwa la kisiasa katika uchaguzi wa Marekani wa mwaka huu wa 2017 uliyokuwa  na ushindani mkubwa, na ni pigo kwa rais Donald Trump aliyemuunga mkono mgombea Roy Moore wa chama cha Republikan, baada ya kusita hapo awali kufuatia madai yanayomkabili ya udhalilishaji wa kingono.

Roy alishindwa kuwashawishi wapiga kura kutokana na kashfa hizo zinazomkabili.

Aidha Doug Jones alichukua kiti hicho cha useneta kwa kujishindia asilimia 49.9 ya kura ikilinganishwa na mpinzani wake Roy Moore alipata asilimia 48.4 , kukiwa na tofauti ya wapiga kura takriban 21,000 kati ya kura milioni 1.3 zilizopigwa.

USA Wahlkampf Alabama Roy Moore in Fairhope (Reuters/J. Bachma)

Mgombea wa chama cha Republikan Jaji Roy Moore

Hii ni kulingana na idadi iliyotangazwa na vyombo vya habari vya Marekani.

Jones aliye na miaka 63 aliwahi kuwa mwendesha mashtaka wa serikali aliyepata umaarifu zaidi baada ya kuwahukumu wanachama wa siasa kali za kibaguzi Ku Klux Klan au KKK waliyoliripua kanisa moja la watu weusi mwaka wa 1960 na kusababisha mauaji ya wasichana wanne.

Jimbo la Alabama lampeleka mwanademokrats ndani ya bunge la Senate la Marekani.

Hata hivyo matokeo ya uchaguzi wa seneti unamueka kwa mara ya kwanza ndani ya robo karne mwanasiasa wa democrat katika jimbo la Alabama ndani ya bunge la Senate la Marekani.

"Kwa kweli nimefurahishwa sana kwa ushindi huu, tumeionyesha nchi namna tunavyoweza kuungana," alisema Jones alipokuwa anawahutubia wafuasi wake katika eneo la Birmingham,  ambapo wafuasi walionekana wakifurahia kwa kukumbatiana.

"Watu wa kizazi changu wanahitaji dunia kuwa tofauti kuliko ilivyo sasa, na uteuzi wa Doug Jones' unathibitisha kuwa dunia inaweza kuwa tofauti kuliko ilivyo sasa," alisema mmoja wa wafuasi wa Jones Nathan Wood House.

USA Wahlen in Alabama (Reuters/M. Gentry)

Baadhi ya wafuasi wa Doug Jones

Naye Arnold Gray mmoja wa wafuasi wa Roy Moore amesema hakushtushwa na ushindi wa Jones lakini anaamini mgombea wake ni mtu wa hekima na angeweza kuwawakilisha watu wa Alabama vizuri.

Jimbo la  Alabama, ambapo Donal Trump alishinda wakatib vwa uchaguzi wa rais  mwaka uliyopita  limekuwa njia katika  panda na saa nyengine limeshindwa kufuata njia sahihi kuwezakusonga mbele, alisema Jones.

Kando na Trump kupata pigo alimpongeza Jones kupitia mtandao wake wa kijamii wa twiter. Aliandika kwamba ushindi ni ushindi, na kwamba chama cha  republican kitajaribu tena kugombea kiti hicho ndani ya muda mchache ujao. Lakini kwa upande wake Roy Moore mwenyewe alikataa kukubali kushindwa, huku akionekana kutaka kura hizo zihesabiwe upya.

Kushindwa kwa Moore kunapunguza wingi wa wanachama wa republican kuwa na wajumbe 51 dhidi ya  49  wa democrats katika baraza la Seneti 100. Wengi wanasema ushindi huu ni pigo kwa Warepublican wanaojitahidi kupitisha sheria za rais Trump Bungeni.

 

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri:    Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com