Afrika Kusini yatuma wanajeshi kukabili magenge hatari
11 Machi 2026
Wanajeshi wa jeshi la ulinzi la Afrika Kusini, wamewasili katika baadhi ya miji jimboni Gauteng leo mchana ili kukabiliana na uhalifu pamoja na uchimbaji haramu wa madini.
Hii inakuja baada ya Rais Cyril Ramaphosa kutangaza mwezi uliopita kwamba jeshi litawekwa katika maeneo yaliyoathiriwa na ghasia za makundi ya uhalifu na shughuli haramu za uchimbaji madini, kusaidia polisi.
Vikosi vya jeshi la ulinzi vimeonekana katika mitaa ya Westbury, Riverlea na maeneo mengine karibu na Johannesburg. Hali ilionekana kuogofya kidogo baadhi ya wakazi, lakini wengi walifurahia ujio wajeshi.
"Ninafuraha sana kwa sababu tumekuwa tukilia ili jeshi lije kutokana na uhalifu wa makundi na zamazama katika eneo letu. Kwa hiyo tunafurahi leo kwamba jeshi lipo karibu nasi."
Mkazi mwingine wa Westbury amesema ujio wa jeshi utawasaidia kupata usingizi.
"Tunajihisi salama sana, na sasa tunaweza kulala kwa utulivu na kufurahia Pasaka kwa amani pamoja na likizo zingine", alisema mkazi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Peter Ngobongo, mkazi wa Alexandra na mtanzania anayefanya kazi ya kusafirisha chakula kupitia Uber Eat, amesema:
"Taarifa hii ni nzuri sana na imetutia moyo, ikizingatia kwamba tunafanya kazi kwa hofu sana; kuna matukio ya kukabwa pikipiki, simu, pengine hata uhai unakuwa hatarini."
"Polisi wamekosa kabisa kufanya kazi zao"
Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wanasema kupeleka jeshi kusaidia polisi ni ishara ya kushindwa kwa serikali. Julius Malema ni kiongozi wa Chama cha wapigania uhuru wa kiuchumi EFF.
''Hii ni uthibitisho kwamba polisi wa Afrika Kusini wamekosa kabisa kufanya kazi zao. Rais anaogopa tu kusema kwamba amepoteza imani na polisi wa nchi hiyo.''
Wakazi wamesema pia kumekuwa na ukaguzi wa magari, kama anavyosema Ali mjomba dereva wa Uber.
"Sasa hivi wanatubana sana polisi, lakini hata hivyo sina uhakika kama uhalifu Afrika Kusini utaisha kwa sababu umekuwepo muda mrefu sana", alisema Mjomba.
Katika robo ya mwisho ya mwaka 2025, polisi walirekodi takriban mauaji 6 351, sawa na wastani wa takriban 70 mauaji kwa siku. Ingawa kiwango hiki kimepungua kidogo ikilinganishwa na mwaka 2024, bado kipo juu sana na sasa wengi wanahoji je, ujio wa jeshi utabadilisha hali? Ni suala la kusubiri na kuona.