Abbas asema serikali ya muungano ya Palestina itajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Abbas asema serikali ya muungano ya Palestina itajiuzulu

Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahammud Abbas ametangaza serikali ya muungano itajiuzulu katika kipindi cha saa ishirini na nne zijazo kufuatia mzozo kuhusu usimamizi wa ukanda wa Gaza.

Serikali ya muungano ya wapalestina ambayo mwisho wake unakaribia

Serikali ya muungano ya wapalestina ambayo mwisho wake unakaribia

Maafisa wa serikali hawajathibitisha tangazo hilo lililotolewa hapo jana na Rais Abbas lakini wamekiri kuwa suala hilo la kujiuzulu kwa serikali limekuwa likijadiliwa kwa miezi kadhaa kutokana na baraza la mawaziri kushindwa kuendesha shughuli zake katika ukanda wa Gaza unaotawaliwa na kundi la Hamas.

Hatua hiyo ya kujiuzulu kwa serikali itakuwa pigo kubwa kwa makubaliano yaliyotiwa saini mwezi Aprili mwaka jana ya kuundwa kwa serikali ya muungano kati ya chama cha Abbas cha Fatah na tawi la kisiasa la kundi la Hamas iliyolenga kukomesha uhasama wa miaka saba kati ya makundi hayo mawili.

Serikali inatarajiwa kujiuzulu leo

Kulingana na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali waliohudhuria mkutano wa baraza la chama cha mapinduzi cha Fatah katika mji wa Ramallah, Rais Abbas ametangaza serikali ya muungano wa Palestina itajiuzulu ndani ya kipindi cha saa ishirini na nne.

Rais wa Palestina Mahmud Abbas na waziri mkuu Rami Hamdallah

Rais wa Palestina Mahmud Abbas na waziri mkuu Rami Hamdallah

Afisa katika ofisi ya Rais amesema Abbas atakutana na waziri mkuu Rami Hamdallah leo mchana. Hata hivyo msemaji wa serikali Ihab Bseiso amesema hana taarifa za kuwepo uwezekano wa kujiuzulu kwa baraza la mawaziri.

Bseiso amesema walikutana hapo jana lakini suala la kujuzulu kwa serikali halikujadiliwa. Hata hivyo amethibitisha kuwa Abbas atakutana leo na Hamdallah kujadili jinsi serikali itakavyoendesha majukumu yake na kuongeza mkutano huo wa leo unatarajiwa kuutatua mzozo uliopo serikalini bila ya kufafanua zaidi.

Baraza la mawaziri la Palestina linalojumuisha wataalamu lilikubaliwa na Fatah na Hamas na kupewa jukumu la kusimamia ukingo wa magharibi na ukanda wa Gaza na hivyo kumaliza miaka saba ya kuwepo tawala tofauti katika maeneo ya wapalestina.

Ukanda wa Gaza ndiyo chanzo cha mzozo

Licha ya makubaliano hayo ya kuunda serikali ya muungano,baraza hilo la mawaziri limeshindwa kutekeleza majukumu yake Gaza ambako kuliharibiwa vibaya na vita vilivyodumu kwa siku 50 kati ya Israel na Hamas mwaka jana.

Majengo katika ukanda wa Gaza yaliyoharibiwa wakati wa vita

Majengo katika ukanda wa Gaza yaliyoharibiwa wakati wa vita

Mwanachama wa baraza la vuguvugu la mapinduzi la Fatah Amin Maqbul amesema serikali itajiuzulu kwani ni dhaifu na hakuna uwezekano kuwa Hamas itairuhusu kufanya kazi katika ukanda wa Gaza, jambo ambalo limezua mzozo kati ya vyama hivyo viwili.

Mchakato wa kuijenga upya Gaza umejikokota kutokana na mvutano huo. Maafisa wa serikali hawajasema iwapo mazungumzo ya kuundwa kwa serikali mpya yataijumuisha Hamas. Kundi la Hamas liliuchukua kwa nguvu ukanda wa Gaza kutoka kwa majeshi ya Abbas mwaka 2007 na kumuacha Abbas kuongoza tu sehemu ya ukingo wa magharibi.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com