Zitto Kabwe akosoa mkakati wa rais Mafuguli kuhusu corona | Matukio ya Afrika | DW | 21.05.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Zitto Kabwe akosoa mkakati wa rais Mafuguli kuhusu corona

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameikosoa vikali serikali ya Rais John Magufuli namna inavyoshughulikia janga la virusi vya corona kwa kusahau sayansi na kujikita katika mbinu nyingine.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini amesema huu siyo wakati wa kujitenga na jumuiya ya kimataifa katika kusaka jawabu la pamoja kuhusu tatizo hilo akionya kwamba kufanya hivyo kunaweza kusababisha maafa katika siku za usoni.

Katika hotuba yake aliyoitoa Alhmisi kwa taifa, Zitto Kabwe ambaye miezi ya hivi karibuni aligonga vichwa vya habari kutokana na ziara yake aliyoifanya katika mataifa ya magharibi amehoji kuhusu kuchelewa kutolewa ripoti ya kamati iliyochunguza mwenendo wa utendaji wa maabara ya taifa, baada ya baadhi ya vipimo vyake kutiliwa shaka.

"Licha ya kuwa tangazo la ubovu wa vifaa lilikuwa wazi kwa umma na dunia, lakini mpaka leo, kamati ile haijaweka wazi taarifa ya uchunguzi wake. Na kutokana na hatua hiyo ya serikali ya Jamhuri ya Muungno wa Tanzania, serikali haijatangaza taarifa ya wagonjwa wa corona tangu tarehe 29, Aprili mwaka huu," alisema Zitto.

Tanzania - Tansanias Präsident John Magufuli

Rais Magufuli ameagiza vyuo vifunguliwe pamoja na kuruhusu shughuli za michezo ziendelee nchini Tanzania, baada ya kusema makali ya covid-19 kupungua.

Jawabu sahihi kupitia sayansi?

Mbali ya hilo, kiongozi huyo wa chama cha ACT Wazalendo amesema jawabu sahihi kuhusu janga la virusi vya corona yanaweza kupatikana kwa kutumia njia za kisayansi. Amesema dunia bado iko njia panda kuhusu nini hatma ya virusi vya corona na duniani kote watu wangali wakipoteza maisha.

Kwa maoni yake anasema siyo jambo la busara kwa taifa kama Tanzania kulegeza mipaka yake wakati majirani zake bado wanaendelea kuimarisha udhibiti ili kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19.

"Uhimizaji mkubwa hivi sasa umejikita katika kuondoa tahadhari zote zilizowekwa awali, na leo tumepata taarifa kwamba vyuo vitafunguliwa na pia michezo itaruhusiwa," amesema na kuomgeza kuwa hii ni hatari sana kwa nchi.

Einweihung eines neuen Flugahfen Terminals durch John Pombe Magufuli Kassim Majaliwa

Rais Magufuli pia aliagiza viwanja vya ndege vifunguliwe na kuwaahidi watalii kwamba hawatatkiwa kuka karantini wakija kuzuru nchini humo.

Mwanasiasa huyo amesema ametilia shaka kuhusu takwimu za ukuaji wa uchumi hasa katika janga hili la virusi vya corona, licha ya jitihada za serikali kuanza kufungua mipaka yake kwa kuwakaribisha watalii wa kigeni na kuahidiwa mafungu ya fedha kutoka jumuiya ya kimataifa.

Waziri Kabudi asema mataifa ya magharibi yako tayari kusaidia

Waziri wa Mambo wa Nje wa Tanzania, Palamagamba kabudi amesema leo kuwa ofisi yake imefanya majadiliano ya mataifa kadhaa ya Magharibi yakiwemo ya Umoja wa Ulaya pamoja na Canada ambayo yameahidi kutoa fedha ili kusaidia kusukuma mbele miradi ya serikali hasa katika wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Rais Magufuli amesema kiwango cha maambukizi ya virusi vya corona kimeendelea kupungua ingawa hajaondoa uwezekano wa kutoweka kabisa kwa janga hilo.

Amedokeza jinsi alivyoridhishwa na kazi ya kukabiliana na maradhi hayo na ameamuru vyuo vya elimu ya juu, wanafunzi wa kidato cha sita na shughuli za michezo yote kurejea katika hali ya kawaida kuanzia Juni Mosi.

Mwandishi: George Njogopa