Yemen yakabiliwa na kitisho cha kugawika tena | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Yemen yakabiliwa na kitisho cha kugawika tena

Yemen inakabiliwa na kitisho kipya cha kugawika tena pande mbili. Wachambuzi wanaamini kuna hofu kubwa ya Yemen kutumbukia katika machafuko makubwa kama inavyoshuhudiwa Afghanistan, Iraq, Libya na Syria.

Jemen Huthi-Befürworter demonstrieren in Sanaa 23.01.2015

Wafuasi wa Houthi wakiandamana katika mji mkuu, Sanaa (23.01.2015)

Wakati Yemen Kaskazini na Yemen Kusini zilipoungana na kuwa nchi moja, Jamhuri ya Kiarabu ya Yemen, mnamo mwezi Mei 1990, gazeti moja la Uingereza liliandika kwa kejeli: "Nchi mbili masikini zimekuwa nchi moja masikini."

Tangu ilipoungana, Yemen imeendelea kuorodheshwa na Umoja wa Mataifa kama mojawapo ya nchi 48 zenye maendeleo madogo kabisa ulimwenguni, nchi masikini kabisa miongoni mwa mataifa masikini inayotegemea kwa kiwango kikubwa msaada wa kigeni na ikijitahidi kuuokoa uchumi wake.

Lakini kufuatia kujiuzulu kwa rais, waziri mkuu na baraza la mawaziri wiki iliyopita, mgogoro wa sasa wa kisiasa, umetishia kuigeuza nchi hiyo kuwa taifa lililoshindwa. Na jambo la muhimu zaidi ni kwamba Yemen pia iko katika hatari ya kugawanyika tena pande mbili, na pengine inaelekea kutumbukia katika vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe.

Charles Schmitz, mchambuzi katika taasisi ya Mashariki ya Kati, amenukuliwa wiki iliyopita akisema, "Tunaangalia jinsi nchi itakavyogawanywa na tunaelekea katika mchakato mrefu wa mashauriano, lakini huenda pia tunaelekea katika vita."

Katika ripoti iliyochapishwa Jumanne wiki hii shirika la kimataifa linaloshughulikia mizozo lilisema kuanguka kwa serikali ya Yemen kumevuruga mchakato wa kukabidhi madaraka na "kunaongeza kitisho cha nchi kugawanyika, uchumi kudorora na machafuko kuenea kama muafaka hautafikiwa hivi karibuni."

Mansur Hadi Präsident Jemen ARCHIV

Rais Abdu Rabbu Mansour Hadi

Kuondolewa madarakani kwa serikali ya rais Abdu Rabbu Mansour Hadi ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa Marekani aliyeshirikiana na nchi hiyo katika mashambulizi ya ndege zisizo rubani dhidi ya kundi la al Qaeda katika rasi ya Urabuni, AQAP, lenye ngome yake katika maeneo ya kusini ya Yemen. Marekani ilikuwa na imani kubwa na mshirika wake kiasi kwamba kujiuzulu kwa serikali "kuliwashangaza maafisa wa Marekani," kwa mujibu wa gazeti la New York Times.

Machafuko makubwa yatarajiwa Yemen

Matthew Hoh, mkufunzi katika Taasisi ya Sera ya Kimataifa, CIP, aliliambia shirika la habari la IPS, "Sijui kama Yemen itagawika pande mbili ama la. Lakini ninaamini hofu kubwa ni Yemen kutumbukia katika machafuko makubwa kama tunavyoshuhudia nchini Afghanistan, Iraq, Libya na Syria, mataifa ambayo yote yamenufaika kutokana na sera ya kigeni ya Marekani ya kuingilia kati kijeshi."

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja wa kiarabu ambaye hakutaka jina lake litajwe, Wahouthi wa Yemen ambao wamenyakua madaraka ni sehemu ya waumini wa dini ya Kiislamu wa madhehebu ya Shia, na inaonekana wanadhaminiwa na Iran. Lakini taifa hilo lina idadi kubwa ya waumini wa madhebu ya Sunni wanaoungwa mkono na nchi jirani ya Saudi Arabia, hali ambayo yumkini ikachochea mzozo wa kimadhehebu, kama vile inavyoshuhudiwa chini Syria, Iraq na Lebanon.

Jemen Huthi-Rebellen 22.01.2015

Waasi wa Houthi (22.01.2015)

Jambo la kinaya ni kwamba Marekani, Saudi Arabia na Iran zote zina adui mmoja; kundi la al Qaeda katika rasi ya Uarabuni, AQAP, ambalo lilidai kuhusika na mauaji ya kiholela katika ofisi za jarida la Charlie Hebdo mjini Paris, Ufaransa mapema mwezi huu. "Kwa kifupi hali nchini Yemen ni mzozo mkubwa wa kisiasa," amesema mwanadiplomasia huyo.

Si rahisi kubashiri kitakachotokea

Vijay Prashad, Profesa wa masomo ya kimataifa katika chuo cha Trinity nchini Marekani, ameliambia shirika la habari la IPS kuwa ni vigumu kubashiri kitakachotokea Yemen wakati huu kwa sababu mikakati ya vita haijakamilika.

Serikali ya Yemen iliyoegemea Marekani imekuwa tangu mwaka 2004 ikifanya mchezo mchafu na Marekani katika vita dhidi ya ugaidi. Kwa upande mmoja serikali ya rais Ali Abdullah Saleh na baadaye rais Hadi, ilipendekeza kwa Marekani kwamba ilikuwa ikilipiga kundi la al Qaeda. Lakini kwa upande mwingine walilitumia suala la al Qaeda kuwawinda na kuwakandamiza maadui, wakiwemo Wahouthi.

Prashad amesema mchezo huu ulijulikana na Wamarekani lakini wakaufumbia macho. Mchezo huu ndio ulioliwezesha kundi la AQAP kuuteka mji wa Jar na maeneo mengine ya Yemen na kuyadhibiti kirahisi. Prashad amepuuzilia mbali madai kwamba Wahouthi ni wawakilishi wa Iran nchini Yemen, akisemani ni muungano wa kikabila ulioonja makali ya upanga wa marais wa zamani Saleh na Hadi.

Mwandishi: Josephat Charo/IPS

Mhariri: Saumu Mwasimba

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com