Wito watolewa kutaka Muasi Kony na wenzake wakamatwe | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.10.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wito watolewa kutaka Muasi Kony na wenzake wakamatwe

Harakati za kundi hilo la waasi wa Uganda-LRA- bado zinaendelea.

default

Kiongozi wa LRA Joseph Kony.

Mwendesha mashitaka katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa mjini The Hague Luis Moreno, ametoa wito tena , kiongozi wa kundi la waasi wa Uganda Lord Resistance Army-LRA-Joseph Kony na makamanda wenzake wakamatwe.

Taarifa ya mahakama hiyo imesema uamuzi wa kutoa wito mwengine wa kukamatwa Kony na makamanda wake, unafuatia mashambulio mapya yaliofanywa na waasi hao dhidi ya raia wasio na hatia katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambako wamo mafichoni. Imearifiwa kwamba tarehe 18 mwezi uliopita, waasi hao wa Uganda walivishambulia vijiji ndani ya Kongo katika wilaya ya Haut Uelé katika eneo la Dungu.

Katika taarifa yake jana mahakama ya uhalifu ya kimataifa yenye makao yake makuu mjini The Hague Uholanzi, ilisema waasi wa LRA walitwaa mali na kuchoma moto majumba, pamoja na kuwakamata kwa nguvu wanafunzi na kuondoka nao. Aidha watu kadhaa pia waliuwawa.

Mtindo wa kuwateka nyara watoto umekua ukitumiwa na waasi hao, ambao huwatumia katika mapigano au kukidhi haja zao kimapenzi. Kwa mujibu wa taarifa maelfu ya watu wamelazimika kutawanyika ili kunusuru maisha yao.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka katika mahakama hiyo ya kimataifa, joseph Kony na makamanda wake Okot Odhiambo na Dominic Ongwen wanapaswa kujibu mashitaka ya uhalifu wa kivita na maovu dhidi ya binaadamu. Taarifa imesema Kony aliyechukua uongozi wa kundi hilo lenye wafuasi wengi kutoka kabila la Acholi 1988, alitoa amri ya kukamatwa zaidi ya watu 1.000 kwa nguvu ili kulitanua jeshi lake. Waranti wa kukamatwa kwao ulitolewa na mahakama 2005.

Kiongozi huyo wa LRA anabebeshwa dhamana ya vita na mauaji katika eneo la kaskazini mwa Uganda kwa miongo kadhaa sasa, ikiwa ni sehemu ya kampeni yake ya kutaka kuanzisha utawala wa kikiristo utakaozingatia amri 10 za Mwenyezi Mungu. waasi hao wanashutumiwa kwa ubakaji, mauaji ya raia na kuwasajili kwa nguvu watoto katika kundi lao na kuwatumia katika uwanja wa mapigano.

Vita kati ya kundi hilo na majeshi ya serikali ya Uganda vimesababisha watu milioni mbili kutawanyika na maelfu kupoteza maisha yao kaskazini mwa Uganda.

Hadi sasa jitihada za amani zimekwamishwa na Kony baada ya mazungumzo yaliofanyika kusini mwa Sudan kushindwa , alipokataa kutia saini makubaliano ya amani akitaka ufafanuizi juu ya hatima yake kutokana na waranti wa mahakama ya kimataifa wa kumtia nguvuni .

Ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo ya kimataifa Bw Moreno, ilizitaka jumuiya za kimkoa na kimataifa kuziunga mkono Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na Uganda katika kuandaa kutiwa nguvuni Kony.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com