1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Zaidi ya watu 900 washukiwa kuambukizwa Ebola DRC

25 Mei 2026

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema zaidi ya watu 900 wanashukiwa kuwa wameambukizwa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/5EHUu
DR Congo Rwampara 2026 | Kituo cha matibabu ya Ebola katika Mkoa wa Ituri baada ya kuchomwa moto
Polisi wa Kongo akilinda kituo cha matibabu ya Ebola katika hospitali ya Rwampara nje kidogo ya BuniaPicha: Gradel Muyisa Mumbere/REUTERS

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema zaidi ya watu 900 wanashukiwa kuwa wameambukizwa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema juhudi za ufuatiliaji zimeongezwa na hadi sasa watu 904 wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola wametambuliwa, huku maabara ikithibitisha zaidi ya watu 100 walioambukizwa.

Nazo mamlaka za maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa AFC/M23 huko mashariki mwa nchi hiyo, zimechukua hatua kali za kuzuia maambukizi zaidi, ambapo watu wote wanaorejea kutoka Bunia na jimbo la Ituri watalazimika kukaa karantini kwa siku 21 kabla ya kuingia mjini Goma.  Dr. Biya Nkizinkiko, ni Mkurugenzi wa afya wa mkoa wa Kivu Kaskazini na alisema kuwa;

"Eneo la Kanyaruchinya litaanza kufanya kazi kuanzia Jumatatu, na kwa kuwa litakuwa tayari linafanya kazi, hata kama vituo vya ukaguzi vimefungwa, watu kutoka maeneo ya Ituri, Beni na Bunia wakifika kwenye vituo vyetu vya forodha, kutakuwepo na wahudumu wa afya ambao watawachunguza na kuwaelekeza katika vituo vilivyotengwa kwa ajili ya karantini."

Ugonjwa huo unaosababishwa na kirusi cha Ebola aina ya Bundibugyo hauna chanjo wala tiba iliyoidhinishwa kwa sasa.