1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 5,000 waliuawa kwenye maandamano ya Iran

18 Januari 2026

Afisa wa Iran aliyeomba kufichwa jina lake amesema mamlaka nchini humo zimethibitisha kuwa watu wasiopungua 5,000 wameuawa katika maandamano ya hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/570pp
Waombolezaji wahuhudhuria mazishi ya maafisa wa vikosi vya usalama waliouawa katika maandamano yenye vurugu
Afisa wa Iran amesema mamlaka zimethibitisha kuwa watu wasiopungua 5,000 wameuawa katika maandamanoPicha: Majid Asgaripour/WANA (West Asia News Agency)/REUTERS

Maafisa wa Iran hawajatoa idadi kamili ya vifo kutokana na maandamano hayo, lakini kundi la haki za binadamu la Iran Human Rights (IHR) lenye makao yake makuu nchini Norway liliripoti kwamba watu 3,428 wamethibitishwa kuuawa na vikosi vya usalama, huku wakionya kwamba idadi halisi inaweza kuwa juu zaidi.

Makadirio mengine yanaweka idadi ya watu waliofariki kuwa zaidi ya 5,000 -- na pengine hadi 20,000, imesema IHR.

Kituo cha upinzani cha Iran International kilicho nje ya nchi kimesema kuwa watu wasiopungua 12,000 waliuawa wakati wa maandamano hayo, kikinukuu vyanzo vya juu vya serikali na usalama.

Mahakama yapinga takwimu

Idara ya Mahakama ya Iran imepinga kabisa takwimu hizo. Maafisa wa Iran wamesema maandamano hayo yalikuwa ya amani kabla ya kugeuka kuwa "machafuko" yaliyojumuisha uharibifu wa mali ya umma.

Mamlaka za Iran zimelaumu hali hiyo kusababishwa na ushawishi wa kigeni, hasa kutoka kwa maadui wake Marekani na Israel.

Siku ya Jumamosi, kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khameneialisema watu "elfu kadhaa" wameuliwa na kile alichokiita "mawakala" wa nchi hizo mbili waliosababisha machafuko. Kulingana na shirika la habari la Iran, Khamenei amesema nchi yake inamwona Trump kuwa mhalifu anayehusika na uharibifu, watu kujeruhiwa na kulichafua taifa lake.

Msemaji wa Idara ya Mahakama amesema mpaka sasa hakuna adhabu yoyote ya kifo iliyotolewa inayohusiana na maandamano hayo. Shirika la habari limemnukuu afisa huyo akisema mchakato wa kutoa adhabu ya aina hiyo ni mgumu na mrefu unaoweza kuchukua muda wa miezi hadi miaka kadhaa.

Huduma za intaneti kurejeshwa 

Watu wa Iran wakitembea kwenye mitaa ya mji mkuu Tehran Januari 15, 2026
Mamlaka za Iran zimesema zinafikiria kurejesha "hatua kwa hatua" huduma za intaneti baada ya kusimamisha mawasilianoPicha: Morteza Nikoubazl/NurPhoto/picture alliance

Mamlaka za Iran zimesema zinafikiria kurejesha "hatua kwa hatua" huduma za intaneti baada ya kusimamisha mawasiliano kote nchini humo zaidi ya wiki moja iliyopita. Haya ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani. Huduma za kupiga simu za kimataifa zilirejeshwa tangu Jumanne, na za kutuma ujumbe mfupi zikarejeshwa Jumamosi asubuhi.

Jumamosi jioni, shirika la habari la Tasnim liliripoti "mamlaka husika zilitangaza kwamba upatikanaji wa intaneti pia utarejeshwa polepole", lakini halikutoa maelezo zaidi.

Likinukuu "chanzo chenye taarifa" ambacho hakikutajwa, shirika hilo lilisema programu za ndani za kutuma ujumbe "zitarejeshwa hivi karibuni" kwenye mtandao wa ndani wa Iran.

Maandamano hayo, yaliyoanza Desemba 28, yameonekana kama changamoto kubwa kwa uongozi wa Iran tangu maandamano ya miezi kadhaa yaliyosababishwa na kifo cha Mahsa Amini mwaka wa 2022.

Chanzo: Mashirika

 

Tanbihi ya Mhariri: Makala hii awali ilijumuisha picha kutoka shirika la SalamPix. Iliondolewa tarehe 12 Machi 2026 baada ya Picture Alliance na Imago kutuarifu kuwa walikuwa wanaondoa picha za SalamPix kutokana na wasiwasi kuhusu chanzo chake na uwezekano wa kuwa zimehaririwa.