Watafiti wagundua mbao yenye umri wa miaka nusu milioni
22 Septemba 2023Kipande hicho cha kipekee cha mbao kilichohifadhiwa vyema kimepatikana katika maporomoko ya maji ya Kalambo yaliyoko kaskazini mwa Zambia karibu na mpaka na Tanzania. Kulingana na utafiti uliochapishwa katika jarida la masuala ya asili, ni kwamba kipande hicho kinasadikika kuwa na umri wa miaka 476,000 kabla ya maendeleo ya Homo Sapiens yani spishi ambayo inajumuisha binadamu wa sasa.
Kifaa hicho cha Mbao chenye alama za kukatwa kinaonyesha kwamba zana za mawe zilitumiwa kuunganisha magogo mawili makubwa ili kutengeneza muundo unaoaminika kuwa jukwaa, njia ya kutembea au kifaa kilichoinuka ili kuwaweka watu juu ya maji. Mkusanyiko wa zana za mbao, ikiwa ni pamoja na kabari na fimbo ya kuchimbia pia vilipatikana katika eneo hilo.
Mababu wa zamani wa binadamu walikuwa tayari wanajulikana kwa kutumia mbao wakati huo, lakini kwa matumizi fulani kama vile kuwasha moto au kuwinda. Larry Barham ambaye ni mtaalamu wa mambo ya kale kutoka Chuo Kikuu cha Liverpool cha huko Uingereza na ambaye pia ni mwandishi mkuu wa utafiti huo, amelieleza shirika la habari la AFP kwamba kwa ufahamu wake, rekodi iliyopita ya mmiliki wa kifaa cha muundo wa mbao ilikuwa na umri wa miaka 9,000.
Barham alisema muundo huo "ulikuwa ni mabadiliko ya ugunduzi" wa mwaka 2019 wakati walipokuwa wakifukua eneo hilo lililopo kwenye kingo za mto Kalambo, mita 235 juu ya maporomoko ya maji. Ugunduzi huo unaojumuisha mbao ya kale ni adimu kwasababu mbao huwa zinaoza na kuacha mabaki kidogo ya kuweza kufuatilia rekodi za kihistoria.
Lakini kiwango kikubwa cha maji katika maporomoko ya maji ya Kalambo ndicho kinaaminika kuwa kimeweza kuhifadhi kipande hicho cha mbao kwa karne kadhaa. Uchimbaji uliofanyika miaka ya 50 na 60 katika eneo hilohilo, uliweza kugundua vipande vya mbao, lakini havikuweza kurekodiwa kwa usahihi.
Hata hivyo mara hii, watafiti wametumia mbinu mpya zinazobaini miaka kwa kupima ni lini mara ya mwisho madini yalipigwa na jua. Hiyo ilidhihirisha kwamba kifaa hicho kilikuwa na umri mkubwa kuliko walivyofikiri watafiti hapo awali takribani miaka nusu milioni. Ushahidi wa mapema wa spishi ya Homo Sapiens unaaminika kuwa karibu miaka 300,000.
Lakini kwa mujibu wa Barham mafuvu ya ndugu wa binadamu Homo heidelbergensis yanayodhaniwa kuwa aliishi kati ya miaka 200,000 hadi 700,000 iliyopita yaligunduliwa katika ukanda huo. Barham anaongezea kwamba ugunduzi wa kifaa hicho cha mbao, umebadili fikra zake kuhusu watu wa kale.
Anasema "walibadilisha mazingira yao ili kurahisisha maisha, hata kama ilikuwa ni kutengeneza tu jukwaa la kukaa kando ya mto kufanya kazi zao za kila siku."
Mtaalamu huyo anasema watu hao wa kale walitumia akili zao, mawazo na ujuzi kuunda "kitu ambacho hawakuwahi kukiona kabla, kitu ambacho hakikuwahi kuwepo awali". Anaongeza kuwa ugunduzi huo unaashiria dhana ya kiwango cha juu cha fikra na "uwezekano wa matumizi ya lugha".
Waandishi wa utafiti huo pia walisema ugunduzi huo unapinga wazo kwamba mababu wa zamani wa binadamu walikuwa wahamaji, kwa sababu muundo huo unaonekana kuwa makao ya kudumu karibu na maporomoko ya maji ambayo ni chanzo cha kudumu cha maji.