1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wa WHO watembelea maabara ya Wuhan

3 Februari 2021

Wataalamu wa shirika la Afya Duniani, WHO, wamefanya uchunguzi kwenye maabara ya mjini wa Wuhan nchini China inayodaiwa na maafisa wa Marekani kuwa chimbuko la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3ooP1
China | WHO Experten in Wuhan
Sehemu ya wataalamu wa WHO wakiwasili kwenye maabara ya mji wa Wuhan.Picha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Ziara hiyo imefanyika wakati matumaini ya kupatikana chanjo yenye ufanisi mkubwa yameongozeka. 

Janga la maambukizo ya virusi vya corona bado halijanaonesha dalili za kupungua duniani, hata baada ya kuanza kutolewa chanjo.

Watu zaidi ya milioni 100 wameambukizwa na zaidi ya milioni 2.2 wameshakufa na kusababisha madhara makubwa katika uchumi wa dunia.

Katika juhudi za kupambana na janga hilo ujumbe wa wataalamu wa shirika la afya duniani umewasili kwenye maabara ya mji wa Wuhan nchini China, ambako baadhi ya maafisa wa Marekani wanadai kuwa chimbuko la virusi vya corona.

Hakuna uwezekano wa kupatikana majibu 

China Wuhan Coronavirus Institute of Virology
Jengo la taasisi ya utafiti wa virusi mjini Wuhan nchini ChinaPicha: Getty Images/AFP/H. Retamal

Wataalamu hao wamekwenda kwenye Taasisi ya Taaluma za Virusi kufanya uchunguzi kwa lengo la kubainisha chanzo cha virusi hivyo.

Virusi vya corona viligunduliwa katika jimbo la Wuhan kwa mara ya kwanza. Ziara ya wataalamu hao inazingatiwa kuwa nyeti kisiasa katika jimbo hilo.

Hata hivyo, mtaalamu mmojawapo Peter Daszaka amesema haielekei iwapo itawezekena kupata majawabu kamili katika muda mfupi wa ziara ya ujumbe wa wataalamu hao.

Hapo awali yalikuwapo madai miongoni mwa maafisa wa utawala wa Trump kwamba virusi vya corona vilitokea kwenye maabara ya jimbo la hilo la Wuhan.

Dunia inaweza kupata chanjo yenye ufanisi

Weltspiegel 02.02.2021 | Serbien Belgrad | Impfstoff aus Russland & China
Picha: Oliver Bunic/AFP/Getty Images

Wakati ujumbe wa shirika la WHO unaendelea na uchunguzi, matumaini ya kupambana kwa ufanisi na maradhi ya corona yameongezeka baada ya kupatikana chanjo ya Urusi ya Sputnik yenye tija ya zaidi ya asilimia 90.

Juu ya chanjo hiyo, mkurugenzi wa kituo cha maradhi ya kuambukiza cha nchini Urusi Alexander Gintsburg amesema "kama jinsi wataalamu wote wanavyofahamu, kwa matokeo kama hayo, pana matumaini makubwa kwamba chanjo hii itakuwa na ufanisi siyo tu wa miezi michache bali ufanisi wa zaidi ya miaka miwili.”


Urusi na nchi nyingine kadhaa zilianza kutoa chanjo mwaka uliopita pakiwepo mashaka juu ya ufanisi wa chanjo hizo.


Wakati huo huo, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema kila chanjo inaungwa mkono na Umoja wa Ulaya na amesema chanjo ya Urusi, Sputnik V inaweza kutumika mara itakapoidhinishwa na wataalamu wa Umoja wa Ulaya.