Warusi wamrudisha Kremlin Putin | Magazetini | DW | 19.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Warusi wamrudisha Putin

Warusi wamrudisha Kremlin Putin

 Ushindi wa Putin katika uchaguzi wa Urusi unazidi kukosolewa baada ya mpinzani wake wa karibu kisiasa, Alexis Navalny, kupigwa marufuku kushiriki na tume ya uchaguzi.Mwaka mmoja madarakani rais Frank-Walter Steinmeier.

 Ushindi wa Vladmir Putin katika uchaguzi wa rais nchini Urusi unazidi kukosolewa na hasa kwa hatua ya mpinzani wake wa karibu kisiasa, Alexis Navalny, kupigwa marufuku kushiriki na tume ya uchaguzi. Vile vile mwaka mmoja madarakani wa Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.

Gazeti la Augsburger Allgemeine  kuhusu ushindi wa Putin.

Licha ya mfumo kandamizi na udanganyifu katika mchakato mzima wa uchaguzi, nchi za Magharibi hazipaswi hata mara moja kujiingiza katika suala hilo. Warusi walio wengi wanasimama pamoja na Putin. Wanavutiwa na ile hali ya kurudi kwa nguvu za kisiasa katika ikulu ya Kremlin. Putin, kwa hivyo, anajua kucheza karata zake kitaifa. Ikiwa umaarufu wake utatosha kiasi cha kwamba rais huyo aliyekaa muda mrefu madarakani kuendelea kung'ara hata panapofanyika uchaguzi wa kidemokrasia, ni suala ambalo hakuna yoyote anayeweza kulijibu. Ikulu ya Urusi inazuia bila kuchoka kejeli na hata changamoto dhidi ya kiongozi wao huyu.

Gazeti la Mannheimer Morgen linasema Putin, mwenye umri wa miaka 65, ni raisi na amepewa mamlaka ya kuendelea kuwa kiongozi na muokozi wa Warusi dhidi ya maadui zao wote katika ulimwengu wa Magharibi.Hata bila ya kuonekana waziwazi udanganyifu katika siku ya uchaguzi, mfumo wa uongozi na mbinu zilizotengenezwa muda mrefu na kiongozi huyo aliyewahi wakati mmoja kuwa jasusi, zilikuwa zikifanya kazi tangu hata kabla ya uchaguzi huu na  ndizo zilizofanikisha lengo bila ya kuonekana matumizi ya nguvu katika kampeni ya kuwashawishi wananchi wengi washiriki katika uchaguzi. Hapana shaka, mbinu hizi ndizo zinazowafanya Warusi wengi kuielewa serikali na kutoitwika mzigo wa lawama.

Reutlinger General-Anzeiger

Na mhariri wa gazeti la Reutlinger General-Anzeiger anasema hatua kwa hatua, Putin anacheza mchezo wa kuifanya Urusi kama mali yake binafsi, kwa kuendelea kujiongezea madaraka. Wakati huo huo kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 65 amezidi kuyafanya mambo magumu kwake mwenyewe na kwa nchi yake kwa kuanzisha muendelezo wa madaraka yake. Hata hivyo, nchi za Magharibi zinapaswa kuelewa kwamba zinabidi kuchagia katika kuleta mageuzi hatua kwa hatua. Na isitoshe, Ulaya ipo katika nafasi nzuri zaidi ya kushirikiana na jirani yake huyo. Katika mapambano ya ushindani duniani, Marekani, China na Urusi zinaweza kuitegemea Ulaya inayojiamini kuchukua dhima ya kuwa msuluhishi. Na hili kwa hakika linawezekana tu ikiwa nchi za Umoja wa Ulaya hazitogawika na kila mmoja kuvutia kwake.

Stuttgarter Nachrichten

Linazungumzia mwaka mmoja madarakani wa rais wa shirikisho, Frank-Walter Steinmeier. Jumatatu hii Steinmeier ametimiza mwaka mmoja tangu kuingia madarakani. Wiki iliyopita alimkaribisha Kansela Angela Merkel na baraza lake la mawaziri na kuwakabidhi nyaraka rasmi za uongozi. Na ikiwa serikali hii bado itakuwa ni imara, basi Steinmeier anaweza kujivunia. Hilo litakuwepo tu endapo wapinzani wa muungano huo wa vyama vikubwa au wanaopendelea migogoro ya kisiasa watakaa kimya, na basi hapo Steinmeier peke yake anaweza kutajwa kwamba amefanikisha.

Mwandishi: Saumu Yussuf
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com