Wapigania demokrasia Hong Kong wapata ushindi wa kishindo | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.11.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wapigania demokrasia Hong Kong wapata ushindi wa kishindo

Uchaguzi wa halmashauri za mitaa umekamilika Hong Kong Jumatatu, huku kiongozi Carrie Lam akikubali kuwa ushindi wa kambi inayounga mkono demokrasia unaashiria wananchi kutoridhishwa na uongozi wa mji huo.

Katika taarifa yake, Lam amesema kwamba kura inaakisi kutoridhika kwa wananchi na hali ilivyo kwa sasa. Ameongeza kwamba serikali itasikiliza kwa unyenyekevu na kutafakari sana juu ya uchaguzi ambao vyama vinavyounga mkono demokrasia vimeshinda kwa wingi katika halmashauri za wilaya zote 18 za jiji hilo na kuwapokonya viti wagombea walizoeleka wa upande unaounga mkono serikali ya China.

Kevin Lam mshindi wa halmashauri ya wilaya ya South Horizons West, amesema ushindi wao ni ujumbe wa wananchi kwa serikali kuu ya China pamoja na viongozi wa Hong Kong.

"Kwamba wapiga kura hawafurahishwi na jinsi serikali inavyoshughulikia waandamanaji hadi hivi sasa. Hususan katika miezi mitano iliyopita, na ukatili wa polisi kwa kweli umekithiri. Na wananchi wa Hong Kong wayatumie matokeo haya kudai demokrasia zaidi siku za mbele," amesema Kevin Lam.

Soma zaidi: Waandamanaji 100 wazingirwa katika chuo kikuu Hong Kong

Ingawa halmashauri za wilaya zinahusika zaidi na masuala ya kijamii, ni miongoni mwa wawakilishi wa kundi la wateule 1,200 watakaomteua kiongozi ajae wa mji huo mwaka 2022.

China yaonya utulivu Hong Kong hautoharibiwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema Hong Kong bado ni sehemu ya China, bila ya kujali kinachotokea katika eneo hilo lenye mamlaka yake ya ndani.

Hongkong Lokalwahlen Regierungschefin Carrie Lam (Reuters/A. Perawongmetha)

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam

Wang ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi habari akiwa mjini Tokyo, Japan. Ameongeza kwamba jaribio lolote la kuharibu utulivu na maendeleo ya Hong Kong haliwezi kufanikiwa.

Akiwa katika mkutano na Wang, Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe amesisitiza juu ya umuhimu wa kuwepo Hong Kong iliyo huru na yenye uwazi, chini ya mfumo wa nchi moja, serikali mbili.

Wakati huo huo, serikali ya Taiwan imesema matokeo hayo yanaonyesha azma ya wananchi ya kutafuta demokrasia na uhuru.

Na nchini Marekani wanasiasa mashuhuri wa vyama vya Democratic na Republican, pamoja na maseneta Marco Rubio na Elizabeth Warren, wameyasifu matokeo hayo.

Matokeo hayo yanaweza kuilazimisha serikali kuu ya China kutafakari tena jinsi ya kushughulikia maandamano, ambayo kwa sasa yanatimiza mwezi wake wa sita.

Waandamanaji wana hasira juu ya kile wanachokiona kama uingiliaji kati wa China wa uhuru ulioahidiwa koloni hilo la zamani la Uingereza wakati liliporudshwa chini ya mamlaka ya China mnamo mwaka 1997.

Soma zaidi: Hong Kong: Maelfu waandamana mitaani kudai uhuru kamili

Vyanzo: (dpa,ap)

Sauti na Vidio Kuhusu Mada

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com