1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji 100 wazingirwa katika chuo kikuu Hong Kong

Daniel Gakuba
20 Novemba 2019

Wanaharakati wa demokrasia wapatao 100 wamenaswa katika jengo la chuo kikuu lililozingirwa na polisi, uwezekano wao kuweza kutoroka ukizidi kupungua. Umoja wa Mataifa umehimiza maridhiano baina ya polisi na waandamanaji.

https://p.dw.com/p/3TN6C
Hongkong Demonstranten versuchen die Polytechnische Universität zu verlassen
Mwandamanaji akijaribu kutoroka kupitia mtaro wa maji machafuPicha: AFP/A. Wallace

Mamlaka ya Hong Kong imearifu kuwa hadi saa tano usiku wa kuamkia leo, wanaharakati wa demokrasia wapatao 800 walikuwa wamekwishaondoka katika jengo hilo la chuo kikuu cha ufundi cha mjini Hong Kong, 300 kati yao wakiwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 18.

Waliobaki ndani ya jengo hilo lililozingirwa na polisi saa 24 kwa siku, wanajaribu kila njia kutoroka. Msichana mmoja aliyejaribu kupita katika mfereji wa maji machafu, amesema amerudi nyuma baada ya kumuona nyoka katika mfereji huo.

Carrie Lam alaani uundaji wa silaha ndani ya chuo kikuu

Hongkong Anti-Regierungs Proteste | Sporthalle als Schlafraum
Ukumbi wa chuo kikuu uliokuwa ukitumiwa na waandamanaji kama maficho yaoPicha: Getty Images/AFP/N. Asfouri

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam amewahimiza vijana wadogo waliomo katika jengo hilo kutoka nje na kukutana na wazazi wao wanaowasubiri. Lakini pia amelaani wale aliosema wanayageuza mazingira ya chuo kikuu kuwa kiwanda cha silaha.

''Inatisha kwa chuo kikuu kimegeuka karakana ya kuunda silaha. Kulingana na taarifa nilizonazo, yamepatikana maelfu ya mabomu ya petroli ambayo hayajatumika, na kemikali zimeibiwa kutoka maabara.'' Amesema Bi Lam na kuongeza kuwa baadhi ya majengo pia yanatumiwa na waandamanaji kufanya mazoezi ya jinsi ya kuwashambulia polisi.

Shirika la habari la Reuters limewaona wanafunzi wapatao mia moja waliorejea nyuma baada ya kushindwa kukimbia kupitia mifereji ya maji. Walikuwa na simulizi za kutisha, wakisema mitaro ilikuwa na harufu mbaya, mende na hata nyoka wakiwa kila mahali.

Hong Kong, kizingiti kingine katika uhusiano wa Marekani na China

Mzozo huu wa maandamano mjini Hong Kong umeleta msuguano kati ya China, ambayo Kisiwa cha Hong Kong kiko chini ya himaya yake, na Marekani inayokosoa jinsi mzozo huo ulivyoshughulikiwa.

Hongkong Proteste
Baadhi ya vijana wadogo walijisalimisha na kuruhusiwa kuondoka baada ya kujielezaPicha: Reuters/A. Abidi

Baraza la seneti mjini Washington limepitisha sheria ya kuunga mkono harakati za demokrasia na haki za binadamu mjini Hong Kong, ambayo inamtaka waziri wa mambo ya nje wa Marekani kusaini agizo la angalau mara moja kila mwaka, linalotaja uhuru wa ndani kisiwa cha Hong Kong, kama sharti la mji huo kuweza kufanya biashara na Marekani.

China imeipinga vikali sheria hiyo, ikisema itafanya kila juhudi kulinda uhuru na mamlaka yake ya utaifa katika mji huo.

Umoja wa Mataifa umeitolea mwito Hong Kong, wa kufanya kila liwezekanalo kupunguza mvutano baina ya polisi na waandamanaji.

rtre, ape