Wapiga kura 53 Milioni wa Misri Wamchagua Rais Mpya | Matukio ya Afrika | DW | 26.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wapiga kura 53 Milioni wa Misri Wamchagua Rais Mpya

Wamisri wameanza kuteremka vituoni kupiga kura katika uchaguzi wa rais utakaofanyika siku mbili ambao mkuu wa zamani wa vikosi vya wanajeshi Abdel Fatah al-Sissi-mpinzani mkubwa wa Udugu wa kiislam anatarajiwa kushinda.

Jemedari mstaafu Abdel Fatah al Sissi

Jemedari mstaafu Abdel Fatah al Sissi

Uchaguzi huo wa rais utakaoendelea kwa muda wa siku mbili unashindaniwa na kiongozi wa zamani wa wanajeshi Abdel Fatah al Sissi na kiongozi wa chama cha mrego wa shoto Hamdeen Sabbahi.Wadadisi wanakubaliana Sabbahi hana nafasi ya kujikusanyia idadi ya maana ya kura.

Jemedari mstaafu el Sissi mwenye umri wa miaka 59 ndie anaeongoza serikali ya mpito iliyoundwa baada ya kumtimua madarakani na baadae kumtia ndani rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasi Mohammed Mursi,miezi kama 11 hivi iliyopita. Zaidi ya hayo Abdel Fatah al Sissi anadhihirika kujivunia imani ya wananchi wengi wa Misri tangu alipovunja nguvu vuguvugu la wafuasi wa Mohammed Mursi wakiwemo pia wafuasi wa Udugu wa kiislam.

Milolongo ya watu wamepiga foleni mbele ya vituo vya uchaguzi vilivyofunguliwa mjini Cairo tangu saa tatu za asubuhi vituo ambavyo vimepangwa kufungwa saa tatu za usiku hii leo.

Wengi wa wananchi wa Misri wanamwangalia Abdel Fatah el Sissi kuwa ndie kiongozi atakaerejesha utulivu baada ya miaka mitatu ya vurugu na mgogoro wa kiuchumi uliofuatia vuguvugu la wapenda mageuzi lililomng'owa madarakani Hosni Mubarak mnamo mwaka 2011.

Shujaa atakaewapatia wananchi mkate wao

Präsidentschaftswahl in Ägypten 26.05.2014

Wapiga kura wanapiga foleni kusubiri zamu yao

Mahmoud al Minyawi,mpiga kura mwenye umri wa miaka 66 anasema "amempigia kura " mzalendo"kwasababu anasema "nchi inahitaji nidhamu katika wakati huu wa shida."

Saber Habib mwenye umri wa miaka 64,mkaazi wa Suez,mashariki ya mji mkuu Cairo anasema "wanamtaka kiongozi mwenye nguvu,kuiongoza nchi na kuwapatia wananchi mkate wao."

Samia Chami ambae ni mfanyakazi wa serikali anasema atampigia kura al Sissi ili kumshukuru kwa kuwaondolea Mursi madarakani.

Matokeo ya uchaguzi kabla ya juni tano

Ägypten Wahlen 26.05.2014

Polisi wamewekwa Kila pembe kuhakikisha uchaguzi unapita salama

Mara baada ya kupiga kura jemedari huyo wa zamani wa Misri, Abdel Fattah al Sissi amesema ulimwengu mzima unawaangalia wamisri wakiandika ukurasa mpya wa historia yao na kuahidi mustakbal mwema kwa nchi yao.Umati wa watu walimkimbilia kuna waliombusu na wengine kumpa mkono.

Wapinzani wake wanahisi akichaguliwa,basi jeshi litakua linathibitisha linaidhibiti nchi hiyo.Mashirika ya haki za binaadam yanasema serikali ya mpito inayoendeshwa na jeshi ni ya kimabavu hata kuishinda ile iliyokuwa ikiongozwa na Hosni Mubarak.

Matokeo ya uchaguzi wa rais yanatarajiwa kutangazwa kabla ya Juni tano ijayo.Uchaguzi wa bunge huenda ukaitishwa msimu wa mapukutiko mwaka huu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu