Wanasayansi Afrika kusini wanachunguza aina mpya ya virusi vya corona | Matukio ya Afrika | DW | 31.08.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wanasayansi Afrika kusini wanachunguza aina mpya ya virusi vya corona

Wanasayansi nchini Afrika Kusini wanafuatilia aina mpya ya kirusi cha corona ambacho polepole kinazidi kusambaa katika miezi ya hivi karibuni, kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kuambukiza NICD.

Aina hiyo, inayojulikana kama C.1.2., iliripotiwa wiki iliyopita na Kituo cha Utafiti cha KwaZulu-Natal.

Ingawa maambukizi mengi Afrika Kuisini yanatokana na kirusi cha aina ya Delta chenye chimbuko lake nchini India, lakini wanasayansi wameanza kutiwa wasiwasi na aina hiyo ya C.1.2 kutokana na kwamba kasi yake ya mabadiliko ni mara mbili ya aina nyingine za virusi ulimwenguni.

Hata hivyo wanasema kasi yake ya maambukizi bado ni ndogo.

Soma zaidi: Ujerumani kusaidia utengenezaji chanjo Afrika Kusini

Wakati wa mkutano wa mtandaoni na waandishi wa habari, mtafiti Penny Moore kutoka NIDC amesema hadi hivi sasa hakuna data za kutosha zinazotokana na utafiti kuthibitisha jinsi gani aina hiyo ya kirusi inaweza kuushambulia mwili wa binadamu. Lakini ameongeza kuwa wana uhakika wa kutosha kuwa chanjo zinazotolewa Afrika Kusini zitaendelea kuwalinda watu dhidi ya ugonjwa huo pamoja na kifo.

Hadi hivi sasa aina hiyo mpya ya virusi vya corona ya C.1.2 imeguduliwa katika majimbo tisa ya Afrika Kusini, pamoja na sehemu nyingine ulimwenguni ikiwa ni pamoja na China, Mauritius, New Zealand na Uingereza.

Hata hivyo hakijasambaa sana hadi kuweza kutangazwa kuwa nia aina yenye hatari zaidi ya kirusi cha corona kama zilivyo aina za Delta na Beta zilizozuka Afrika Kusini mwaka uliopita.

Schulbeginn Weltweit Südafrika

Watoto wakipimwa joto la mwili kabla ya kuingia darasani, Cape Town, Afrika Kusini.

Taifa liloathirika zaidi Afrika

Afrika Kusini ni nchi iliyoathirika zaidi na virusi vya corona barani Afrika. Tangu janga hilo kuanza ulimwenguni, Afrika Kuisni imeripoti maambukizi ya watu milioni 2.7 na vifo 81,830.

Kirusi aiana ya Beta kilisababisha wimbi la pili la maambukizi mnamo mwezi Desemba na Januari, na taifa hilo hivi sasa linapambana na wimbi la tatu lilosababishwa na aina ya Delta ambalo linatarajiwa kuendelea kuwepo na kugongana na wimbi lijalo la nne.

Soma zaidi: Afrika ina idadi kubwa ya watu wanaougua COVID-19

Richard Lessells, mtaalam wa magonjwa ya kuambukiza na mmoja ya waandishi wa utafiti juu ya C.1.2, amesema kuibuka kwake kunatudhihirishia kwamba janga hili halijakwisha na kwamba virusi hivi bado vinatafuta njia bora za kuendelea kutuambukiza.

Wakati huo huo kampeni ya kutoa chanjo ya nchini Afrika Kusini bado inaendelea kwa kasi ndogo, kwani ni asilimia 14 ya idadi jumla ya watu waliochanja hadi sasa.

Vyanyo: afp,rtre