1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati Tanzania wataka adhabu ya kifo ifutwe

Florence Majani10 Oktoba 2023

Wadau wa haki za binadamu, wanasheria na taasisi za kimataifa nchini Tanzania wamehimiza kufutwa kwa adhabu ya kifo wakihoji inakwenda kinyume na haki za binadamu, japo haijatekelezwa kwa takribani miaka 30 sasa.

https://p.dw.com/p/4XMXP
Wanaopinga hukumu ya kifo Tanzania wanasema inakwenda kinyume na haki za binadamu.
Wanaopinga hukumu ya kifo Tanzania wanasema inakwenda kinyume na haki za binadamu.

Wadau wa haki za binadamu, wameitaka serikali ya Tanzania kuondoa adhabu ya kifo na badala yake kuwe na sheria mbadala, wakihoji kuwa adhabu hiyo inakiuka misingi ya haki za binadamu.

Maazimio yao yametolewa wakati dunia ikiadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga adhabu hiyo. Akizungumza katika kongamano hilo, Rais wa chama cha wanasheria cha Tanganyika, TLS, Harold Sungusia amebainisha.  

Imeelezwa katika kongamano hilo kuwa, mara ya mwisho Tanzania kutekeleza adhabu ya kifo ni mwaka 1994 na hilo limepelekea wafungwa wanaotumikia adhabu hiyo kubaki wakiwa na sintofahamu juu ya hatma ya maisha yao.  

Kongamano hili linafanyika wakati hivi majuzi, Oktoba saba, mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe ikiwahukumu watu tisa kunyongwa hadi kufa, kwa kosa la kuua ndugu wawili.

Ghana ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo tayari zimefuta adhabu ya kifo.
Ghana ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo tayari zimefuta adhabu ya kifo.Picha: Xinhua/IMAGO

Ghana na Zambia zimefuta adhabu ya kifo

Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Ulaya, Christine Grau alitoa orodha ya nchi ambazo tayari zimefuta adhabu ya kifo zikiwamo Zambia na Ghana huku akitaka majadiliano hayo kuwa mapana zaidi katika muktadha wa kikanda na kitaifa ili kupata suluhisho bora.

"Ni muhimu kwetu kuelewa kwamba hukumu ya kifo ni sawa na kukubali kushindwa, na mhusika anabaki bila malipo yoyote, licha ya uhalifu mbaya alioufanya, mwanadamu na asili yake haviwezi kuondolewa kwa hukumu ya mahakama bado mtenda kosa anabakia kuwa mmiliki binafsi wa haki za binadamu,” amesema Christine Grau.

Kwa upande wake, Waziri wa Sheria na katiba Tanzania, Dk Pindi Chana, amesema wakati akifungua kongamano hilo kuwa  Tanzania ipo katika mapitio ya sheria hiyo ya adhabu ya kifo.

Mbiu ya mnyonge: Idadi ya watu walionyongwa mwaka 2022 yaongezeka

Wakati wadau hao wakidai adhabu hiyo ifutwe wapo wanaopinga kufutwa kwa adhabu hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Ana Henga, wakitaka iendelee kutumika ili kuwawajibisha wahalifu. 

Hukumu za kifo 691 zilitolewa mwaka 2022

Ripoti ya Tume ya Haki Jinai, iliyotolewa mwaka huu imeeleza kuwa watu 691 walihukumiwa kunyongwa mwaka 2022 lakini kukiwa hakuna utekelezaji wowote.

Itakumbukwa kuwa Sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16 imeainisha makosa yanayopelekea mtu kupewa adhabu ya kifo kuwa ni pamoja na mauaji ya makusudi, na  uhaini. Sheria hii ilitungwa 1945, na ilianza kufanya kazi Septemba 28 septemba 1945.

Mwandishi: Florence Majani. Dar es Saaam