1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Polisi Somalia yasema makabiliano na Al Shabaab yamemalizika

15 Machi 2024

Nchini Somalia ripoti iliyotolewa na jeshi polisi imesema kuwa makabiliano ya risasi yaliyodumu kwa zaidi ya saa 13 na wanamgambo wa Al Shabaab mjini Mogadishu yamemalizika na sasa hali ya usalama imerejea.

https://p.dw.com/p/4dbtX
Somalia | SYL- Mogadishu
Polisi nchini Somalia wakiwa mbele ya hoteli ya SYL iliyoshambulia a wanamgambo wa Al ShabaabPicha: Farah Abdi Warsameh/AP Photo/picture alliance

Nchini Somalia ripoti iliyotolewa na jeshi polisi imesema kuwa makabiliano ya risasi yaliyodumu kwa zaidi ya saa 13 na wanamgambo wa Al Shabaab mjini Mogadishu yamemalizika na sasa hali ya usalama imerejea.

Milio ya risasi imesikika tangu jana usiku mjini Mogadishu baada ya wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab kuishambulia hoteli ya SYL iliyopo karibu na makazi ya raisi na ofisi ya waziri mkuu.

Soma zaidi Marekani yatangaza vikwazo dhidi ya 'mtandao wa al-Shabaab' 

Duru za kiusalama na mashuhuda wamesema tukio hilo lilitokea kuanzia majira ya saa tatu usiku kwa saa za nchini Somalia baada ya watu wenye silaha kuivamia hoteli ya SYL huku wakifyetua risasi.

Somalia | SYL- Mogadishu
Polisi wa Somalia wakiwa mbele ya hoteli ya SYL ambayo imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na Al ShabaabPicha: Farah Abdi Warsameh/AP Photo/picture alliance

Akizungumza na Shirika la Habari la AFP, Abdirahim Yusuf ambaye ni afisa wa polisi amesema washambuliaji wote wameuawa baada ya mapambano ya  zaidi ya masaa 13 na sasa hali ya utulivu imerejea huku maafisa wakiendelea kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo.

Bado hakuna taarifa rasmi

Pamoja na kumalizika kwa tukio hilo lakini bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na serikali kuhusu vifo ama majeruhi wa tukio hilo ingawa mashuhuda wanasema wameshuhudia magari mawili ya kubebea wagonjwa yakiwa yamebeba watu waliojeruhiwa katika mkasa huo.

Kwa miaka ya karibuni kumekuwa na mfufulizo wa mashambulizi ya namna hiyo mjiniMogadishu, Hoteli hii hii iliyovamiwa ya SYL ilishambuliwa pia mwaka 2019. Mwaka uliopita watu sita waliuawa katika hoteli nyingine ya Mogadishu.

Somalia Militants Twitter
Kundi la wanamgambo wa Al Shabaab limekuwa likifanya uasi dhidi ya serikali ya shirikisho ya Somalia kwa maiak 16Picha: picture alliance / AP Photo

Agosti mwaka 2022, watu 21 waliuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa baada ya kuzingirwa kwa saa 30 kwenye hoteli ya Hayat, miezi miwili baada ya tukio hilo watu wengine 100 walipoteza maisha katika milipuko miwili ya magari mjini Mogadishu

Soma zaidi: Somalia yatangaza makubaliano ya usalama, uchumi na Uturuki

Shambulio la jana linakuja siku chache baada ya serikali ya Marekani kuwawekea vikwazo watu na mashirika 16 katika pembe ya Afrika na mashariki ya kati ambayo yanashotumiwa kwa utakatishaji fedha kwa ajili ya kundi hilo la wanamgambo.

Kwa zaidi ya miaka 16, wanamgambo wa Al-Shabaab wanaofungamana na kundi la itikadi kali la al-Qaeda wamekuwa wakiendesha uasi dhidi ya serikali ya shirikisho ya Somalia inayotambuliwa kimataifa.  Mara nyingi wamekuwa wakizilenga hoteli ambazo hutembelewa na maafisa wa ngazi za juu wa Somalia na wa kigeni.