1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa kupambana na rushwa Afrika wakutana Tanzania

Charles Ngereza,2 Oktoba 2018

Moja kati ya mambo yanayoangaziwa katika mkutano huo ni vipimo vya kuweza kutambua viwango vya mafanikio juu ya vita dhidi ya rushwa.

https://p.dw.com/p/35sT6
Südafrika Protest gegen Korruption ARCHIV
Picha: picture-alliance/dpa/K. Ludbrook

Wakuu wa vyombo vinavyopambana na rushwa barani Afrika na taasisi za kikanda za umoja huo pamoja na asasi za kiraia wamekutana jijiiini Arusha nchini Tanzania na kuzindua mjadiliano dhidi ya vita vya rushwa katika Afrika .

Moja kati ya mambo yanayoangaziwa na mkutano huo ni vipimo vya kuweza kutambua viwango vya mafanikio juu ya vita dhidi ya rushwa ambayo imekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo na kuchochea uwepo wa migogoro ya kijamii na kisiasa barani Afrika .

Waziri wa ofisi ya rais utawala bora nchini Tanzania George Mkuchi ndiye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano ambaye aliwataka viongozi na watendaji mbalimbali wa Afrika wanaoshughulika na masuala ya vita dhidi ya rushwa kuchukua maamuzi na mapendekezo mbalimbali katika vita dhidi ya rushwa kivitendo, ili Afrika iweze kuondokana na rushwa ambayo ni chanzo cha migogoro ya kiuchumi na kisiasa.

Rushwa bado ni tatizo kubwa

Wajumbe wa mkutano huo katika majadiliano wamesema rushwa bado ni tatizo kubwa na kuzinduliwa kwa majadiliano hayo ni sehemu ya kuendelea kwa jitihada za kupambana na tatizo hilo ambalo limeeendelea kusababisha kuongezeka kwa umasikini na upatikanaji wa huduma duni za kijamii.

Rushwa imetajwa kuwa chanzo cha migogoro ya kiuchumi na kisiasa.
Rushwa imetajwa kuwa chanzo cha migogoro ya kiuchumi na kisiasa.Picha: DW/Said Michael

Wajumbe hao wanasema rushwa imekuwa ni kikwazo kikubwa cha kukua kwa demokrasia na masuala ya kijamii na uchumi katika mataifa mbalimbali ya Afrika na mali nyingi za umma zimekuwa zikiporwa kwa njia ya rushwa na hivyo mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda muhimu inayopaswa kupewa kipaumbele na kila nchi mwanachama wa umoja wa Afrika.

Umuhimu wa mkutano huo katika kupambana na rushwa Afrika

Dkt. Alfred Sabahene ambaye ni mhadhiri kutoka chuo kikuu cha St. John nchini Tanzania akihudhuria mkutano huo wa siku tatu amesema kuwa mkutano huo una umuhimu mkubwa kutokana na vitendo vya rushwa kushamiri katika bara la Afrika.

Akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa bodi ya ushauri kuhusu vita dhidi ya rushwa barani Afrika Marom Begoto amesema kuwa bodi hiyo imefanya kazi kubwa ikiwemo ya kuishauri umoja wa Afrika mbinu bora za kukabili masuala ya rushwa.

Mkutano huo ni matokeo ya maamuzi ya wakuu wa nchi za umoja wa Afrika mwezi Januari mwaka huu ambao kwa pamoja walitangaza mwaka 2018 kuwa mwaka wa kupambana na rushwa.

 

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman