1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waingereza wapiga kura katika uchaguzi mkuu

Daniel Gakuba
12 Desemba 2019

Raia wa Uingereza wanapiga kura leo katika uchaguzi mkuu wa tatu katika muda usiotimia miaka mitano. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa chama cha Conservative cha waziri mkuu Boris kinao uwezekano wa kushinda.

https://p.dw.com/p/3UgBJ
Großbritannien London  Parlamentswahlen
Waingereza wamejitokeza kupiga kura licha ya baridi na mvuaPicha: picture-alliance/NurPhoto/B. Zawrzel

Licha ya baridi kali na mvua za rasharasha, mistari mirefu ya wapigakura inaonekana katika vituo vya kupigia kura nchini kote Uingereza. Vituo katika majimbo yote 650 ya England, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini vimefunguliwa saa  moja asubuhi, na vinatarajiwa kufungwa rasmi saa nne usiku, majira ya Uingereza. Waziri Mkuu Boris Johnson amepiga kura mjini London, akisindikizwa na mbwa wake.

Viongozi wa kisiasa wametumia mtandao wa twitter kuwahimiza watu kwenda vituoni na kuvichagua vyama vyama. Boris Johnson wa Conservative amesema hii ni fursa ya kuhakikisha kwamba mchakato wa Brexit unakamilika, na katika ujumbe wake wa kuhitimisha kampeni hapo jana, aliwataka Waingereza kuweka kando tofauti zao na kumwezesha kulitimiza hilo.

UK Wahlen 2019 l Premierminister Johnson mit seinem Hund Dilyn vor der Wahlstation in London
Waziri Mkuu Boris Johnson alifika kituoni akisindikizwa na mbwa wakePicha: picture-alliance/empics/J. Brady

''Bila kujali mtazamo wako, bila kujali kama uliunga mkono kubaki au kuondoka katika Umoja wa Ulaya, huu ni wakati wa kuja pamoja na kusonga mbele, na kuheshimu matakwa ya watu wa nchi hii.'' Amehimiza Johnson.

Corbyn awajia juu matajiri

Kwa upande wake kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn, amesema kura kwa chama chake ni kura ya kumaliza sera ya kubana matumizi. Katika ujumbe wake wa kukamilisha kampeni, Corbyn alisema katika maeneo yote aliyokwenda, alitetea maslahi ya watu wa kawaida.

Amesema, ''Ujumbe ulikuwa ule ule, tunataka haki, tunataka haki na fursa sawa. Hatutaki nchi inayoendeshwa na matajiri na mabilioni, na kuwasahau wengine.''

UK Wahlen 2019 l  Labour Party,  Jeremy Corbyn vor der Wahlstation in London
Jeremy Corbyn, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, LabourPicha: Reuters/L. Niesner

Uchunguzi wa maoni ya wapiga kura unampa nafasi kubwa Johnson na chama chake cha Conservative kupata ushindi, lakini matokeo rasmi ndiyo yatakayoonyesha ikiwa ataweza kupata viti vya kutosha kupitisha maamuzi yake bungeni.

Vyama vidogo vyaweza kuwa na turufu kibindoni

Ikiwa Johnson atashindwa kupata wingi huo, wachambuzi wa siasa za Uingereza wanazungumzia uwezekano wa vyama vidogo kupata kura ya turufu, juu ya kuamua namna ya utawala utakaoundwa kutokana na ushirikiano wa kivyama.

Vyama hivyo ni pamoja na chama cha kiliberali, Liberal Democrats kinachoongozwa na Bi Jo Swinson, ambacho kimeshikilia msimamo imara wa kutaka kuibakisha Uingereza ndani ya Umoja wa Ulaya, na hivyo kinaweza kuvutia wapiga kura wasiopenda mchakato wa Brexit.

Katika uchaguzi uliopita mwaka 2017, chama cha Censervative kililazimika kushirikiana na chama cha DUP cha Ireland ya Kaskazini, kuweza kupata viti vya kutosha kuunda serikali.

afpe, ape