1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za lala salama nchini Uingereza

11 Desemba 2019

Wanasiasa nchini Uingereza wanafanya ziara za lala salama katika siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi unaofanyika kesho Alhamisi wakati kura za maoni zikionesha matokeo bado hayatabiriki. 

https://p.dw.com/p/3Uaaf
TV-Duell im Wahlkampf in Großbritannien | Johnson gegen Corbyn
Waziri Mkuu Boris Johnson (Kushoto) na Kiongozi wa Labor, Jeremy Corbyn Picha: picture-alliance/dpa/AP/Itv

Waziri mkuu wa chama cha Conservative Boris Johnson na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Labor, Jeremy Corbyn wanalenga kufanya mikutano mifupi mifupi kwenye maeneo yenye ushindani mkali kujaribu kwa mara ya mwisho kuwavutia wapiga kura.

Johnson mwenye miaka 55 amepanga kuanza kampeni ya nyumba kwa nyumba ya kugawa maziwa huko Yorkshire kaskazini ya Uingereza na kuhitimisha kampeni yake mjini Essex kaskazini mashariki ya London.

UK Wahlen l Wahlkampfveranstaltung bei der JCB Baufirma - Boris Johnson
Picha: Reuters/T. Melville

"Ujumbe wangu kwa wapiga kura wote ambao bado hawajaamua ni kwamba unaweza kuchagua matumaini" amesema Johnson muda mfupi kabla ya kuanza ziara yake ya kampeni.

Corbyn amepangiwa kuwa na mikutano mjini Middlesbrough kaskazini mashariki ya Uingereza akiutaja uchaguzi wa siku ya Alhamisi kuwa muhimu kwa kizazi cha sasa.

Msoshalisti huyo mwenye miaka 70 amesema iwapo atachaguliwa anapanga kuongeza matumizi ya serikali katika huduma za jamii, kutaifisha sekta muhimu na kuitisha kura nyingine ya maoni kuhusu suala la Brexit.

Wahifidhina bado wanaweza kupata ushindi

UK-Wahlen | Jeremy Corbyn
Picha: picture-alliance/empics/S. Rousseau

Kura za maoni zinakiweka mbele chama cha Consivative kuwa kitapata wingi wa hadi viti 28 katika bunge lenye nafasi 650, lakini hiyo ni pungufu ya makadirio ya mwezi Novemba yaliyotabiri ushindi wa chama hicho ungepindukia wingi wa viti 68.

Matarajio ni kwamba chama cha Conservatives kitapata viti 339 ambayo ni ziada ya viti 22 ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2017 huku chama cha upinzani Labour kitapata viti 231 ikiwa ni pungufu ya viti 31.

Katika kura ya maoni ya umma iliyoendeshwa na kampuni ya YouGov imeonesha kwamba Chama cha Scotland SNP kinaelekea kuongeza wabunge 6 na kufikia viti 41 huku waliberali wanatarajiwa kujipatia viti 15 ambayo ni nyongeza ya wabunge watatu.

Paundi yatikisika kutokana na hofu ya uchaguzi

UK-Wahlen | Boris Johnson
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. McKay

Wakati hayo yakijiri sarafu ya Uingereza, Paundi, imenguka leo kwa alama kadhaa kutokana na hofu ya wawekezaji juu ya matokeo ya uchaguzi mkuu.

Sarafu ya Uingereza ilikuwa imara kwa miezi kadhaa iliyopita kutokana na kuongezeka matumani kwamba chama cha waziri mkuu Johnson kitapata ushindi wa wazi katika uchaguzi wa Disemba 12 na kumaliza mkwamo wa Brexit.

Uchaguzi mkuu wa mapema nchini Uingereza uliitishwa ili kumaliza mkwamo wa mchakato wa Brexit unaikabili nchi hiyo tangu kura ya maoni ya mwaka 2016 iliyoamua ijitoe kutoka Umoja wa Ulaya.

Baada ya kushindwa kuongoza serikali isiyo na wingi bungeni, waziri mkuu Johnson anatumai kupata serikali mpya yenye wingi wa viti itakayomwezesha kuitoa nchi yake kutoka Umoja wa Ulaya mnamo Januari 31 2020.