Wabunge Marekani wapuuza ombi la Snowden | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wabunge Marekani wapuuza ombi la Snowden

Wabunge wenye ushawishi mkubwa katika bunge la Marekani wametupilia mbali ombi la aliyekuwa mfanyakazi wa shirika la taifa la usalama la Marekani, NSA, Edward Snowden kutaka msamaha.

Mvujishaji wa siri za Marekani Edward Snowden ukimbizini mjini Moscow

Mvujishaji wa siri za Marekani Edward Snowden ukimbizini mjini Moscow

Wabunge hao walieleza msimamo wao kuhusu Edward Snowden katika mahojiano na kituo cha televisheni cha CBS jana Jumapili. Mwenyekiti wa kamati inayohusika na ujasusi katika seneti ya Marekani Dianne Feinstein alisema kuwa badala ya kuvujisha siri kwenye vyombo vya habari, Snowden angetoa malalamiko yake kwa siri kwenye kamati anayoiongoza.

''Alikuwa na nafasi, kama alitaka kufichua maovu, kuipigia simu kamati ya ujasusi ya baraza la wawakilishi na ya seneti, na kusema kwamba anazo taarifa ambazo angependa tuzifahamu. Hakika tungekutana naye, kwa pamoja, au kila kamati kwa wakati wake. Lakini hakufanya hivyo, na sasa baada ya kusabaisha matatizo makubwa kwa nchi yake, anataka msamaha. Jibu langu ni hapana.'' Alisema Feinstein.

Dianne Feinstein, mwenyekiti wa kamati ya ujasusi katika seneti ya Marekani

Dianne Feistein, mwenyekiti wa kamati ya ujasusi katika seneti ya Marekani

Naye mwenyekiti wa kamati ya ujasusi katika baraza la wawakilishi Mike Rogers, amesema kumpa msamaha Edward Snowden ni kitu kisichowezekana.

Alisema, ''Kama anataka kurudi nyumbani, na kuwajibika kwa makosa yake ya kuiba taarifa za siri na kukiuka kiapo chake, nitafurahi kuzungumza naye. Lakini anapaswa kuwajibika kwa yale matendo yake na kama anataka kutoa sababu ya kuchukua hatua hiyo, hii ndio njia sahihi ya kufanya hivyo.

Njia sahihi ya kulalamika

Mike Rogers aliongeza kuwa iwapo Snowden anaamini kuwa yapo mapungufu katika mfumo wa ujasusi wa Marekani ambayo alihitaji kuyaweka wazi, haikuwa busara kufanya hivyo kwa njia ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya wanajeshi wa Marekani walio katika operesheni mahali kama Afghanistan.

Hans-Christian Stroebele, mbunge wa Ujerumani aliyekutana na Snowden

Hans-Christian Stroebele, mbunge wa Ujerumani aliyekutana na Snowden

Majibu hayo ya wabunge wa Marekani yametolewa siku chache baada ya mkutano kati ya Snowden na mbunge wa chama cha watetezi wa mazingira cha Ujerumani, Hans-Christian Ströbele mjini Moscow. Baada ya mazungumzo hayo, Snowden alimpa Stroebele barua ambamo alieleza kuwa tayari kutoa ushahidi mbele ya bunge la Marekani, kuweka wazi kile alichokiita ''uhalifu ambao huenda ni mkubwa''.

Tangazo la ukweli

Katika barua hiyo ya ukurasa mmoja, Edward Snowden anaomba msamaha kwa mashitaka dhidi yake, kwa shutuma kuwa alivujisha taarifa nyeti za Shirika la NSA kwa vyombo vya habari.

Mbunge Stroebele alikutana na Snowden Alhamis iliyopita, kuzungumza naye kuhusu taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari, kwamba NSA iliidukua simu ya mkononi ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Snowden aliahidi kutoa maelezo mbele ya bunge la Ujerumani, ikiwa usalama wake utahakikishwa.

Taarifa zilizovujishwa na mfanyakazi huyo wa zamani wa NSA, zimesababishwa miito ya nchi washirika kuacha kudukuana, na zimeanzisha mchakato katika bunge la Marekani kutaka mfumo wa ujasusi wa nchi hiyo ufanyiwe marekebisho.

Katika kile kilichoitwa ''tangazo la ukweli'', ambalo lilichapishwa na gazeti la Der Spiegel la Ujerumani, Edward Snowden alisema udukuzi wa mawasiliano ya halaiki ya watu unaweka kitisho kwa uhuru wa watu kujieleza katika jamii ya kidemokrasia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DW English website/rtre/afpe/ap

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com