1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Hongkong Protest gegen China & Ausschreitungen
Picha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Waandamanaji Hong Kong wapambana na polisi

Grace Kabogo
20 Oktoba 2019

Maandamano ya kuipinga serikali Hong Kong yamegeuka na kuwa ghasia baada ya polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji.

https://p.dw.com/p/3RbPG

Maandamano hayo yamefanyika licha ya makabiliano ya hivi karibuni kati ya polisi na waandamanaji. Umati mkubwa wa waandamanaji uliingia kwenye barabara za wilaya ya Kowloon siku ya Jumapili, wengi wakiwa wamefunika nyuso zao na kukiuka sheria iliyowekwa ya kupiga marufuku watu kufunika uso katika mikutano ya umma.

Polisi kutoka kituo cha polisi cha Tsim Sha Tsui walitumua pia mizinga ya maji dhidi ya maelfu ya waandamanaji. Waandamanaji pia walirusha chupa za mabomu yaliyotengenezwa kwa petroli kwenye lango la chuma la kuingilia katika kituo cha polisi na mbele ya eneo la kituo hicho.

Hongkong Protest gegen China & Ausschreitungen
Waandamanaji wakirusha mabomu ya petroli nje ya kituo cha polisiPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Waandamanaji hao pia waliwasha moto mbele ya maduka mbalimbali na kwenye vituo vya treni na kuweka vizuizi vya barabarani. Watu waliokuwa kando ya barabara walilitoroka eneo la machafuko wakati magari kadhaa ya polisi yakionekana kuingia huko na polisi kuanza mara moja kuondoa vizuizi vilivyowekwa na waandamanaji.

Wiki ya 20 ya maandamano

Hong Kong imeingia katika wiki yake ya 20 ya maandamano yasiokuwa na dalili ya kusitishwa. Wakati wa maandamano hayo walikuwa wakiimba nyimbo na kuonyesha mabango yaliyoonyesha bendera ya China kama nembo ya Swastika iliyotumiwa wakati wa utawala wa Wanazi.

Matthew Lee, mwanafunzi wa chuo kikuu amesema bado ana nia thabiti ya kuendelea kuandamana hata baada ya zaidi ya miezi minne. ''Nawaona baadhi ya watu wakitaka kusalimu amri, lakini mimi sitofanya hivyo kwa sababu Hong Kong ni nyumbani kwangu, tunataka kuilinda hii sehemu, kuilinda Hong Kong,'' alisisitiza Lee.

Hongkong Protest gegen China & Ausschreitungen
Polisi wakitumia maji ya kuwasha dhidi ya waandamanajiPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Kabla ya maandamano hayo Hong Kong iliimarisha ulinzi, ilizuia baadhi ya huduma za treni apmoja na kufunga huduma za umma, huku viongozi wanaotetea demokrasia wakiwatolea wito wananchi kushiriki katika maandamano licha ya kuwepo hatari ya kukamatwa.

Polisi walizuia maandamano kwenye wilaya ya Kowloon kutokana na wasiwasi wa usalama wa umma na mahakama ilisema eneo la maandamano ambalo ni kituo kikubwa cha kubadilisha reli na China bara kiko katika hatari ya kushambuliwa na kuharibiwa.

Soma zaidi: Hofu ya vurugu zaidi yaongezeka Hong Kong 

Hata hivyo, waandaaji wa maandamano hayo waliapa kuendelea na maandamano ingawa bado yamepigwa marufuku na polisi, kwa sababu katiba ya Hong Kong inawahakikishia haki ya kuandamana. Figo Chan, makamu mwenyekiti wa vuguvugu la kutetea haki za binaadamu linaloandaa maandamano hayo anasema sio kwa sababu polisi haijawapa kibali cha kuandamana, basi hawapaswi kufanya hivyo. Amesema hata kama wamekataa ombi lao, watahakikisha watu wengi wanaandamana.

Hongkong Protest gegen China & Auslieferungsgesetz
Maelfu wakiandamana kudai demokrasia Hong KongPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Siku ya Jumamosi polisi walimkamata mwanaume mwenye umri wa miaka 22 kwa tuhuma za kuhusika na shambulizi la kisu dhidi ya kijana ambaye alichomwa kisu na kujeruhiwa wakati akigawa vipeperushi.

Mwanaharakati maarufu wa kutetea haki za binaadamu, Jimmy Sham alishambuliwa na wanaume waliokuwa na visu mwanzoni mwa juma, shambulizi ambalo wabunge wanaotetea demokrasia wamesema lilipangwa ili kuwatisha waandamanaji.

Waandamanaji hao wanajaribu kutoa shinikizo kwa serikali kuyatekeleza madai yao, ambayo yanajumuisha kupatikana kwa tume kamili ya demokrasia na itakayokuwa huru kwa lengo la kuchunguza madai ya ukatili unaofanywa na polisi.

(DPA, AP, AFP, Reuters)