1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu ya vurugu zaidi yaongezeka Hong Kong

Amina Mjahid
1 Oktoba 2019

Hofu ya kupanuka kwa mgogoro zaidi mjini Hong Kong inaongezeka baada ya mmoja ya waandamanaji kijana kupigwa risasi na polisi.

https://p.dw.com/p/3QaUv
Hongkong 70 Jahre Volksrepublik China - Proteste
Picha: Reuters/T. Siu

Hili linajiri wakati maelfu ya watu wakijiunga na maandamano ya kuipinga serikali, yaliosambaa katika eneo hilo linalotawaliwa na China, huku viongozi wa kikomunisti nchini China kuadhimisha miaka 70  ya uwepo wao madarakani.

Msemaji wa Polisi mjini humo Yolanda Yu amesema risasi iliyofyetuliwa na polisi aliyezingirwa na waandamanaji ilimpata kijana huyo katika upande wa kushoto wa kifua chake.

Bi Yolanda amewaelezea waandamanaji kama wafanya vurugu na kusema polisi aliyefyatua risasi alihofia maisha yake wakati alipozingirwa na waandamanaji. Msemaji huyo wa polisi aliongeza kuwa kijana aliyejeruhiwa alipelekewa hospitalini kwa matibabu zaidi  bila ya kutoa taarifa zaidi.

Mwanaharakati Lee Cheuk-yan aliyeongoza maandamano, amesema walitaka kukionesha chama cha kikomunisti kwamba hawana lolote la kusheherekea. Amesema wanaomboleza kwamba baada ya miaka 70 ya utawala wa chama hicho bado wananchi wa Hong Kong na China wananyimwa haki zao za kidemokrasia.

Uingereza yakemea utumiaji wa risasi za moto dhidi ya waandamanaji

Großbritannien Dominic Raab Außenminister
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Dominic Raab Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Grant

Mara kadhaa polisi mjini humo walizoea kufyatua risasi hewani za kuwaonya waandamanaji, lakini hii ni mara ya kwanza kwa mwandanamaji kupigwa risasi.

Hata hivyo katika mkanda wa video uliosambaa katika mitandao ya kijamii inamuonesha polisi akifyatua risasi kwa waandamanaji waliokuwa wanamkrabia huku wengine wakionekana kumgonga gonga afisa huyo katika mkono uliokuwa na silaha akitumia kifimbo cha chuma.

Baadae polisi walirusha vitoa machozi kwa maeneo tariban sita na kutumia maji ya kuwasha mjini humo wakati waandamanaji wakaugeuza mji huo kuwa uwanja wamapambano. Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Uingereza Dominic Raab amesema utumiaji wa risasi za moto dhidi ya waandamanaji mjini humo ni jambo lisilokubalika.

Katika taarifa yake Raab amesema hatua hiyo inahatarisha kutokea vurufu zaidi mjini humo huku akiongeza kuwa tukio hilo linaonyesha umuhimu wa kuwa na mazungumzo ya kina kushughulikia matakwa ya wananchi wa Hong Kong. Amesema wanahitaji kuona uvumilifu na kupungua kwa mvutano kati ya waandamanaji na pia serikali.

Vyanzo: afp, ap,reuters