1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia kujadili usalama katika mkutano wa Munich

Saumu Mwasimba
16 Februari 2024

Vita vya Israel Gaza,hali ya Ukraine na mustakabali wa NATO ni miongoni mwa ajenda zitakazohodhi majadiliano ya siku tatu Kusini mwa Ujerumani

https://p.dw.com/p/4cTA8
Mkutano wa usalama wa Munich
Viongozi katika mkutano wa usalama wa MunichPicha: William Noah Glucroft/DW

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres atafungua rasmi mkutano wa 60 wa kimataifa wa usalama mjini Munich, katika wakati ambapo ulimwengu unakabiliwa na migogoro kadhaa mikubwa.

Kiasi viongozi 50 wa dunia wanatarajiwa kushiriki mkutano huo unaoanza leo Ijumaa.

Viongozi wa ngazi za juu wa kisiasa, maafisa wa kijeshi pamoja na Wanadiplomasia kutoka nchi mbali mbali za ulimwengu waanaanza kukutana leo mjini Munich kwa siku tatu kujadiliana juu ya masuala mbali mbali ya kiusalama na ambayo zaidi yanatarajiwa kugubikwa hasa na suala la vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza pamoja na hali nchini Ukraine.

Agenda

Khofu ya washirika wa jumuiya ya kujihami ya NATO kuhusu msimamo wa Marekani juu ya kutoa ulinzi kwa wanachama wa jumuiya hiyo, pia ni agenda nyingine inayotegemewa kutawala mkutano huo. Marekani inawakilishwa na makamu wake wa rais Kamala Harris ambaye anatarajiwa kuhutubia mkutano huo, huku Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakipangiwa kutoa hotuba zao Jumamosi.

Rais wa Israel Isaac Herzog pamoja na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Israel Kart pia wanashiriki sambamba na wajumbe wa ngazi za juu kutoka Mamlaka ya ndani ya wapalestina itakayowakilishwa na wazi wake mkuu Mohammad Shtayyeh ,Saudi Arabia, Qatar, Misri na Jordan.

Yatafanyika pia majadiliano mengine pembezoni mwa mkutano huo kuhusu hali inayoweza kujitokeza baada ya uchaguzi wa Novemba 5 nchini Marekani na hasa ikiwa rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump atarudi tena madarakani.

Faisal Bin Farhan Al Saud na  Annalena Baerbock
Mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia na UjerumaniPicha: Sven Hoppe/AFP/Getty Images

Soma pia: Israel, Iran zashambuliana Mkutano wa Usalama wa MunichWasiwasi miongoni mwa mataifa ya ulimwengu na hasa yale ya barani Ulaya washirika wa Muungano wa kijeshi wa NATO yana khofu kubwa lifuatia matamshi yaliyotolewa na Trump wiki iliyopita yanayoonesha kwamba kiongozi huyo hatokuwa tayari kuzilinda nchi zitakazoshindwa kuchangia vya kutosha bajeti ya ulinzi katika jumuiya hiyo.

Ujumbe wa bunge la Marekani  kwenye mkutano huo wa Munich umejumuisha zaidi ya wanasiasa 30 wakiwemo wanachama wa chama cha Republican cha bwana Trump. Maafisa wa Urusi na Iran hawakualikwa katika mkutano huo wa 60 wa kujadili masuala ya kimataifa kuhusu ulinzi na diplomasia unaofanyika katika mji wa Munich Kusini mwa Ujerumani.

Mikutano ya pembezoni

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza  David Cameroon ambaye pia anashiriki kwenye mkutano huo amesema kutakuwa na kikao cha pembezoni cha maafisa wa nchi za Umoja wa Ulaya waliosaidia kuwachangia Wapalestina katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na wajumbe wa nchi kubwa za kiarabu na Ghuba kujadili kuhusu mustakabali wa watu wa Israel na Wapalestina ikiwa yatafikiwa makubaliano ya kumalizwa vita.

Wajumbe walioshiriki mkutano wa usalama wa Munich mwaka 2023
Wajumbe kwenye mkutano wa usalama wa Munich wa mwaka 2023Picha: William Noah Glucroft/DW

Mkutano huu unafanyika katika wakati ambapo vita katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 28,000 na Waisrael 1,430. Huku vikiingia mwezi wake wa tano na bado hakuna dalili ya kumalizika vita hivyo.

Mkutano huo pia utajadili migogoro inayoshuhudiwa katika pembe ya Afrika,ongezeko la ukosefu wa chakula na mamilioni ya walioachwa bila makaazi kufuatia migogoro pamoja na suala la mahusiano kati ya nchi za Magharibi na China.