Viongozi duniani walaani shambulizi la Manchester | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi duniani walaani shambulizi la Manchester

Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani leo wameelezea kushtushwa na tukio la mlipuaji wa kujitoa mhanga huko Manchester, Uingereza, lililopelekea vifo vya watu 22 wakiwemo watoto waliokuwa wamehudhuria tamasha la muziki.

Tamasha hilo lilikua la mwanamuziki wa Marekani Ariana Grande. Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, alilitaja tukio hilo kama la kigaidi na lenye kushtusha na akafutilia mbali kampeni yake huku uchaguzi wa Juni 8 ukiwa unakaribia. Mkuu wa upinzani nchini humo Jeremy Corbin alifuata nyayo za May kwa kusimamisha kampeni aliyokuwa ananuia kufanya.

Iwapo tukio hili litathibitishwa kuwa la kigaidi, basi litakuwa baya zaidi nchini Uingereza tangu walipuaji wa kujitoa muhanga walipowauwa watu 52 mjini London katika treni tatu za chini ya ardhi na basi mwezi Julai mwaka 2005.

Mkuu  wa  polisi  mjini  Manchester  Konstebo Ian Hopkins alisema, polisi  inaamini , katika  wakati  huu, shambulio hilo  limefanywa  na  mtu  mmoja , ambapo  alisema umuhimu  umewekwa  katika kutambua  iwapo  alikuwa peke  yake au ni sehemu  ya  mtandao mpana.

Urusi kuongeza ushirikiano wa kigaidi na Uingereza

Viongozi kadhaa duniani wameelezea kushtushwa na  shambulio hilo.

Mjini Berlin Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameandika katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter akisema, "shambulizi hili la kigaidi litazidi kuongeza azma yetu ya kushirikiana na wenzetu Waingereza dhidi ya wale wanaopanga na kufanya matukio hayo ya kinyama. Nawahakikishia Waingereza, Ujerumani iko pamoja nanyi," alisema Merkel.

Palästina PK Trump und Abbas (Reuters/J. Ernst)

Rais wa Marekani Donald Trump amelaani tukio hilo pia

Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema yuko tayari kuongeza ushirikiano dhidi ya ugaidi na Uingereza baada ya tukio hilo na kusema anataraji wahusika hawatakwepa adhabu. Rais wa Marekani Donald Trump aliye ziarani huko Mashariki ya Kati baada ya kukutana na rais wa Palestina Mahmoud Abbas, alikilaani kitendo hicho akisema maisha ya vijana wasio na hatia yamefikishwa kikomo na watu ambao hawana mwelekeo maishani.

"Hili ndilo nililokuwa nikizungumzia katika siku chache zilizopita katika ziara yangu. Jamii yetu haiwezi kuvumilia umwagikaji wa damu unaoendelea," alisema Trump, "hatuwezi kuvumilia hata kidogo kuuwawa kwa watu wasio na hatia, na katika shambulizi la leo watoto wasio na hatia wameshambuliwa pia. Magaidi na wale walio na misimamo mikali pamoja na wafadhili wao ni sharti waangamizwe."

Wasiojulikana waliko wanatafutwa katika mitandao ya kijamii

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alielezea kushtushwa kwake na alisema anapanga kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Uingereza huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisema serikali yake inalaani vikali shambulizi hilo la kigaidi.

Akizungumza bungeni Jumanne, Waziri Mkuu wa Australia Malcolm Turnbull alisema hili ni shambulizi dhidi ya vijana na uhuru wao kote duniani.

"Hili tukio, hili shambulizi, ni baya sana na la kihalifu na la kutisha sana kwasababu linaonekana hasa kuwalenga vijana." alisema Turnbull. "Hili ni shambulizi kwa wasio na hatia. Kwa kweli hakuna uhalifu mbaya zaidi kuliko kuwauwa watoto."

Wanaotumia mitandao ya kijamii wanasaidia kuwatafuta wale ambao hawajulikani walipo kwa kusambaza majina na picha katika mitandao hiyo kwa kauli ya "missing in Manchester".

Großbritannien Anschlag in Manchester (Getty Images/D. Thompson)

Waliohudhuria tamasha hilo wanasindikizwa kutoka eneo la tukio

Serikali ya mji wa Manchester pamoja na Meya wake Andy Burnham ni miongoni mwa waliokuwa wakisambaza kauli hiyo na Burnham alisema mambo yataendeela kama kawaida katika mji huo leo.

"Ni vigumu sana kuamini yaliyotokea hapa katika saa chache zilizopita na kuelezea kwa maneno mshtuko, hasira na uchungu tulio nao. Hawa walikuwa ni watoto, vijana na familia zao ambao walilengwa na magaidi," alisema Burnham. "Hili lilikuwa tukio baya. Fikra zetu ziko na familia wale waliofariki na kujeruhiwa na tutafanya lolote tuwezalo kuwasaidia. Tunaomboleza leo lakini tuko imara."

Mwanamke mmoja kutoka Jamhuri ya Czech aliyekuwa katika tamasha hilo la mziki alisema waliokuwa wanahudhuria hawakufanyiwa ukaguzi wa kile walichobeba.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFP/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com