Vikosi vya waasi nchini Kongo vyarudi nyuma | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 20.11.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Vikosi vya waasi nchini Kongo vyarudi nyuma

Wapiganaji wa jenerali muasi wa Kitutsi Laurent Nkunda, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,jana jioni walianza kuondoka mstari wa mbele wa mapigano.

A man reach out to help two displaced children cross sharp lava rock in a camp for displaced people, Thursday, Nov. 13, 2008, in Kibati just north of Goma in eastern Congo. The city of Goma has been besieged by rebels loyal to renegade Gen. Lauren Nkunda since he reached the outskirts of the provincial capital, and the rebels have promised to fight any African troops that aid the Congolese army.(AP Photo/Karel Prinsloo)

Watoto wakimbizi kwenye kambi ya Kibati kaskazini mwa Goma.

Vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa MONUC vinavyosimamia eneo hilo,vinatumaini kuwa hatua hiyo itafungua njia ya kufanywa majadiliano ili kumaliza mgogoro wa majuma kadhaa katika Wilaya ya Kivu ya Kaskazini.

Kurudi nyuma kwa vikosi hivyo kumetoa matumaini kuwa mapigano ya takriban kila siku yaliyokuwa yakiendelea tango majuma kadhaa kati ya waasi,majeshi ya serikali na wanamgambo wa kiienyeji yatatulia.Kwa mujibu wa msemaji wa vikosi vya Umoja wa Mataifa Luteni Kanali Jean-Paul Dietrich,waasi walianza kuondoka Kanyabayonga na Rwindi jana jioni.Hata mashahidi waliokuwa njiani kwenye barabara kuu inayopitia Kivu ya Kaskazini wamesema,waasi wamehamia kama kilomita 33 kutoka kusini mwa Kanyabayonga.

Nkunda anaeshikilia kuwa na majadiliano ya ana kwa ana pamoja na Rais Joseph Kabila kuhusu mustakabali wa Kongo,aliviamuru vikosi vyake kurudi nyuma,baada ya kukutana na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo mnamo mwishoni mwa juma lililopita.Nkunda ameahidi kuheshimu makubaliano ya kuweka chini silaha na kushiriki katika majadiliano ya amani chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Waasi wamerudi nyuma,kusini ya maeneo waliyoteka na walikovitimua vikosi vya serikali kaskazini mwa mji mkuu wa Wilaya ya Kivu ya Kaskazini Goma.Lakini wangali wakishikilia vituo muhimu kiasi ya kama kilomita 15 kaskazini ya Goma karibu na Kibati.Mapigano ya majuma yaliyopita, mashariki mwa Kongo yamesababisha maafa makubwa ya kibinadamu baada ya maelfu ya watu kukimbia makwao.Mashirika ya misaada yamekuwa yakitoa misaada ya chakula na dawa kwa zaidi ya wakimbizi 200,000 waliokusanyika Kibati na ukingoni mwa Goma.Maelfu wengine wamenasa porini na milimani walikokimbilia kujiepusha na mapigano. Mashirika ya kiraia na yasio ya kiserikali nchini Kongo yamepeleka barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,kuomba vikosi vya amani MONUC mashariki mwa Kongo viimarishwe kwa haraka,ili raia waweze kulindwa kwa ufanisi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamia kupigia kura mswada wa azimio lililopendekezwa na Ufaransa kupeleka Kongo wanajeshi ziada ili kuimarisha vikosi vya MONUC kufikia 20,000.Hivi sasa Umoja wa Mataifa ina wanajeshi 17,000 kulinda amani mashariki mwa Kongo.Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Jean-Maurice Ripert amesema,vikosi hivyo viwe na ufanisi zaidi na vile vile uwezo wake utumiwe kikamilifu kukabiliana na changamoto.

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com