1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Uturuki vyaudhibiti mji wa Afrin

Iddi Ssessanga
18 Machi 2018

Rais wa Uturuki amesema vikosi washirika vya Syria vimetwaa udhibiti kamili wa mji wa katikati mwa jimbo la Afrin, ambao ulikuwa shabaha ya mashambulizi ya miezi miwili ya Uturuki dhidi ya kundi la wapiganaji wa Kikurdi.

https://p.dw.com/p/2uXwp
Türkische Armee rückt in Afrin ein
Picha: Reuters/K. Ashawi

Rais Recep Tayyip Erdogan alisema bendera ya Uturuki na bendera ya wapiganaji wa upinzani wa Syria zimepandishwa katika mji huo, ambao hapo awali ulikuwa unadhibitiwa na kundi la wapiganaji wa Kikurdi linalojulikana kama Vikosi vya Ulinzi wa Raia, au YPG.

"Magaidi wengi walikuwa tayari wamekimbia," alisema Erdogan akiwa katika jimbo la magahribi mwa Uturuki la Cabakkale. Uturuki inavichukulia vikosi vya Kikurdi katika jimbo la Afrin lililoko mpakani mwake na Syria kuwa magaidi wenye mafungamano na kundi lililopigwa marufuku la 'Chama cha Wafanyakazi wa Kikurd' au PKK, ambalo limeendesha uasi ndani ya Uturuki kwa zaidi ya miongo mitatu.

Ankara ilianzisha operesheni dhidi ya mji wa Afrin na maeneo jirani Januari 20, na taratibu ilianza kuwasukumiza wapiganaji na mamia ya raia katikati mwa mji. Wanajeshi wasiopungua 46 wa Uturuki wameuawa katika operesheni hiyo.

Afisa wa Kikurdi, Hadia Yousef, aliliambia shirika la habari la Associated Press kuwa wapiganaji wa YPG hawajaukimbia mji huo, lakini waliwaondoa raia waliobakia "kutokana na mauaji." Alisema mapigano yalikuwa yanaendelea katika mji huo.

Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza lilisema vikosi vinavyoungwa mkono na Uturuki vimechukuwa udhibiti wa nusu ya mji huo, huku mapambano makali yakiendelea.

Türkische Armee rückt in Afrin ein
Mwanajeshi wa Uturuki akipandisha bendera ya nchi hiyo mjini Afrin, baada ya jeshi la Uturuki na vikosi vya jeshi huru la Syria (FSA) kuchukuwa udhibiti kamili wa mji huo Machi 18,2018.Picha: picture-alliance/AA

Shirika hilo linasema karibu watu 200,000 wameikimbia Afrin katika siku za karibuni kuepuka mashambulizi makali ya ndege, na kuingia eneo jirani lililoko chini ya udhabiti wa serikali ya Syria. Televisheni ya Syria ilionyesha picha siku ya Jumapili, za msafara mrefu wa magari na raia watembeayo kwa miguu wakiondoka Afrin. Erdogan amesema wakaazi wa Afrin watarejea.

Safishasafisha ya mabomu

Jeshi la Uturuki wakati huo liliarifu kupitia mtandao wa twitter kuwa lilikuwa linaendesha operesheni za kutafuta mabomu ya ardhini pamoja na miripuko. jeshi liliweka video kwenye mtandao wa kijamii ikimuonesha mwanajeshi aliebeba bendera ya Uturuki na mwanaume anaepeperusha bendera ya upinzani wa Syria kwenye roshani jengo la bunge la wilaya, huku kukiwa na kifaru kilichoegeshwa mtaani.

Mwanajeshi huyo aliitaja hatua ya kutekwa kwa jimbo la Afrin kuwa zawadi kwa taifa la Uturuki na kwa wanajeshi waliouawa katika kumbukumbu ya ushindi maarufu wa vita kuu vya kwanza vya dunia. Picha za shirika binafsi la habari la Uturuki la Dogan, zilionesha wapiganaji wa Syria wakifyatua risasi hewani kusherehekea ushindi.

Tovuti za habari za Kikurdi zilionesha picha za wapiganaji wakiharibu sanamu inayoashiria sherehe za mwaka mpya wa Kikurdi zinazofanyika wiki hii. Sanamu hiyo ni ya Kawa, ambaye ni shujaa wa kubuniwa katika milima ya Zagros nchini Iran aliemshinda mtawala katili na kuwasha mioto kueneza habari, za kuanza kwa majira ya machipuko.

Türkische Armee rückt in Afrin ein
Wanajeshi wa Uturuki na Jeshi Huru la Syria wakiwa katika roshani ya jengo la bunge la mji wa Afrin, Machi 18,2018.Picha: Reuters/K. Ashawi

YPG limekuwa mshirika muhimu wa Marekani katika mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu, na liliteka maeneo makubwa kaskazini na mashariki mwa Syria kutoka kwa wapiganaji wa kundi hilo la itikadi kali kwa msaada wa mashambulizi ya ndege za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani.

Lakini Erdogan amesema mara kwa mara kwamba mshirika wa NATO Uturuki haitoruhusu kuwekwa njia ya magaidi kwenye mpaka wake. Uturuki pia inahofia kuanzisha kwa eneo la utawala wa Kikurdi nchini Syria, ambalo linaweza kuihamasisha jamii yake ya Wakurdi wachache kudai mamlaka zaidi.

Wakurdi ndiyo kundi kubwa zaidi la kikabila lisilo na utaifa katika kanda ya Mashariki ya Kati, ambapo karibu watu milioni 30 wa jamii hiyo wakiishi katika eneo lililogawika kati ya Iran, Iraq, Uturuki na Syria.

Wapigani wa Kikurdi na shirika la uangalizi wa haki za binadamu walisema ndege za Uturuki zilishambulia hospitali kuu ya Afrin siku ya Ijumaa, na kuuwa zaidi ya dazeni moja ya watu. Jeshi la Uturuki hata hivyo limekanusha madai hayo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Sylvia Mwehozi