Venezuela yaishutumu Marekani kwa 'wizi wa waziwazi'
11 Desemba 2025
Katika taarifa yake, serikali ya Venezuela imeeleza kwamba itatetea "uhuru wake, rasilimali zake za asili, na heshima ya kitaifa kwa msimamo mkali kabisa.” Imeongeza kwamba itawasilisha malalamiko yao kwa mashirika ya kimataifa.
Rais wa Marekani Donald Trump alithibitisha kukamatwa kwa meli hiyo mapema jana Jumatano, hatua iliyosababisha bei ya mafuta kupanda na kuongeza mvutano kati ya Washington na Caracas.
Kukamatwa kwa meli hiyo kunakochukuliwa kama juhudi za karibuni za utawala wa Trump kuongeza shinikizo kwa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ambaye ameshtakiwa kwa makosa ya biashara haramu ya dawa za kulevya na ugaidi.
Wavenezuela wagawanyika juu ya hatua za Trump
Wavenezuela katika eneo la Florida Kusini hata hivyo wamegawanyika kuhusiana na hatua zinazofuata za Rais Donald Trump, wakati Marekani ikiendelea kupeleka vikosi zaidi vya kijeshi na kuzishambulia boti kutokea angani
Watu wengi walioko ughaibuni wanatamani kupata kiongozi mpya kuchukua nafasi ya Rais Nicolas Maduro nchini Venezuela, nchi ambayo maelfu wamekimbia kutokana na mgogoro wa kiuchumi na kisiasa katika miaka ya hivi karibuni.
"Ikiwa kuna hisia moja ya kawaida miongoni mwa Wavenezuela wote, ni chuki tuliyo nayo dhidi ya Chavismo na Maduro," alisema Andrea Gonzalez, mwenye umri wa miaka 38, akimaanisha itikadi ya mrengo wa kushoto iliyopewa jina la mtangulizi wa Maduro, marehemu Hugo Chavez.
Tofauti zaibuka kuhusu jinsi ya kumwondoa Maduro
Baadhi wanasema matumizi ya nguvu ndiyo chaguo pekee, hasa baada ya Maduro kujitangaza tena kuwa rais mwaka 2024 katika uchaguzi ambao ulionekana kugubikwa na udanganyifu.
Lakini wengine, wanaohofia uharibifu unaoweza kusababishwa na vita, wanataka kutumia njia za kidiplomasia.
Ingawa utawala wa Trump umesema unawalenga "magaidi wa dawa za kulevya," wengi wanahoji nia ya kweli ya Washington ya kuingia ghafla kijeshi katika nchi hiyo ya Amerika Kusini yenye akiba kubwa ya mafuta duniani.
'Upanga ukatao pande zote'
Maduro kwa muda mrefu amedai kwamba Washington inakusudia kumpindua. Na huko Doral, karibu na Miami, ambapo zaidi ya asilimia 40 ya wakazi wana asili ya Venezuela, Diana Gonzalez anaamini kwamba huo ndio ukweli.
Mbunifu huyo wa mapambo ya ndani mwenye umri wa miaka 47 anaunga mkono uingiliaji kati wa "asilimia 100" katika nchi yake ili kuipindua serikali anayoituhumu kwa ufisadi, kuvuruga uchaguzi na kuwakandamiza wapinzani.
Baada ya miaka mingi ya majaribio ya amani ambayo hayajafanikiwa, hilo ndilo chaguo pekee linalowezekana, alisema.
"Hatuwezi kuendelea peke yetu kwa sababu ni mapambano yasiyo ya haki kati ya watu waliobeba bendera dhidi ya watu wenye silaha," alisema, akiongeza kwamba "hakuna mtu yeyote nchini Venezuela atakayepigania utawala."
Lakini kwenye eneo hili la Doral, wengi hujiepusha kuzungumzia suala hilo na pia wengine hawapendi kumzungumzia Trump.
Hatua ya serikali ya Trump ya kuwakamata wahamiaji wengi wa asili ya Amerika ya Kusini baada ya kufuta Hadhi ya Ulinzi wa Muda (TPS) iliyotolewa kwa Wavenezuela wapatao 600,000 chini ya utawala wa rais aliyepita Joe Biden imeathiri pakubwa jamii hiyo. Na hilo limesababisha mvutano.
Andrea Gonzalez, anayeunga mkono mipango ya Trump nchini Venezuela lakini anakosoa sera zake za uhamiaji nchini Marekani, baada ya yeye binafsi kupitia kadhia hiyo.
Hata hivyo, anaamini kwamba Trump anaweza kurejesha imani katika jamii yake ikiwa atafanikiwa kumpindua Maduro.