1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela: Upande wa upinzani wahimiza maandamano zaidi

Zainab Aziz
12 Februari 2019

Upande wa upinzani nchini Venezuela umeitisha maandamano  zaidi leo Jumanne kwa ajili ya kulishinikiza jeshi la nchi hiyo liruhusu kuingia ndani ya nchi misaada iliyotolewa na Marekani,

https://p.dw.com/p/3DC6M
Venezuela Juan Guaido
Picha: Getty Images/AFP/Y. Cortez

Maadamano hayo yanalaaniwa vikali na Rais Nicolas Maduro ambaye anasema ni njama za kutaka kuivamia Venezuela. Idadi kubwa ya raia wa Venezuela leo wanatarajiwa kushiriki kwenye maandamano kuishinikiza serikali iruhusu kuingia nchini humo tani 100 za misaada, ambayo imezuiwa kwenye mpaka kati ya Venezuela na Colombia.

Harakati za Rais wa mpito aliyejitangaza Juan Guaido, zilizowezesha kupatikana kwa misaada hiyo zinaonekana kuwa ni mtihani mkubwa katika mapambano ya kisiasa kati yake na Rais Maduro. Kiongozi huyo wa upinzani wa Juan Guaido, alisema siku ya Jumatatu kwamba wamefaulu kuwasilisha misaada ya kwanza japo kwa kiwango kidogo.

Guaido, ambaye pia ni spika wa bunge mwezi uliopita alitambuliwa na mataifa mengi ya Magharibi kama rais wa mpito wa Venezuela, alichapisha picha yake kwenye mtandao wa Twitter akionekana kuzunguukwa na magunia na mitungi myeupe ya virutubisho lakini hakusema ilikotoka misaada hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: picture-alliance/AP Images/R. Drew

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa mwito mpya kwamba yuko tayari kusaidia ili kuutatua mgogoro wa Venezuela wakati alipofanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Jorge Arreaza alipokutana naye mjini New York. Umoja wa Mataifa unataka yafanyike mazungumzo ya kisiasa kati ya pande hizo mbili ili kuinusuru nchi hiyo ya Amerika ya Kusini isitumbukie zaidi kwenye vurugu.

Katika hali hiyo ya vuta nikuvute ya nchini Venezuela Rais Maduro ametangaza kwamba atakabiliana na maandamano yaliyoitishwa na upande wa upinzani kwa kuongoza maandamano ya vijana wa mrengo wa kushoto katikati ya mji mkuu, Caracas, ambako serikali imesema itakusanya saini za watu ambao wanampinga Rais wa Marekani Donald Trump.

Mvutano kati ya serikali na upinzani nchini Venezuela unahusu misaada ya kibinadamu na iwapo itaruhusiwa kuingia katika nchi hiyo ambayo uchumi wake umezorota na ambayo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, dawa na mahitaji mengine ya misingi.

Kwa muda wa siku tano sasa, misaada ya chakula na dawa imelimbikizana kwenye vituo kadhaa vya kukusanya misaada vilivyopo karibu na mpaka kati ya Colombia Venezuela. Daraja la kisasa linalounganisha miji miwili ya mpakani limefungwa kwa kuwekwa makontena na malori yenye manenki ya kubeba mafuta.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/DPAE

Mhariri: Yusuf Saumu