Uvumilivu kwa Korea Kaskazini umekwisha, Tillerson | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uvumilivu kwa Korea Kaskazini umekwisha, Tillerson

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson amesema Sera ya uvumilivu wa kimkakati kwa Korea Kaskazini imefikia mwisho. Waziri Tillerson amesema hayo katika ziara yake nchini Korea Kusini.

USA Außenminister Rex Tillerson | Vereidigungszeremonie (Reuters/C. Barria)

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson

Waziri Tillerson aliongeza kuwa mbinu kadhaa zinabuniwa ili kukabiliana na taifa hilo lililotengwa.

Tillerson alitembelea mpaka ulio na ulinzi mkali zaidi duniani Ijumaa DMZ, jambo linalomfanya kuwa mmoja wa maafisa wakuu wa Marekani waliotembelea na hata kupigwa picha katika eneo hilo.

Mpaka huo wa DMZ umelindwa pande zote mbili, kukiwa kumetegwa vilipuzi, uzio wenye makali ya wembe, mitego na maelfu ya walinzi waliojihami. Zaidi ya vilipuzi milioni moja vinaaminika kuzikwa katika mpaka huo.

Alipokuwa akizungumza mjini Tokyo awali, waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani aliapa kuweka mikakati mikali ili kukabiliana na kitisho cha nyuklia cha Korea Kaskazini. Lakini hakusema zaidi kuhusiana na yatakayojumuishwa kwenye mwelekeo huo mpya utakaotolewa na Marekani.

Miaka 20 ya diplomasia imeshindwa kuishawishi Korea Kaskazini

"Nataka pia kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wetu wa kihistoria, ushirikiano wetu wa kiuchumi unaozidi kuongezeka na kama ulivyosema, muungano wetu madhubuti wa usalama, kama jawabu kwa kitisho kinachoongezeka cha Korea Kaskazini," alisema Tillerson.

Südkorea Explosion in der entmilitarisierten Zone (DMZ) (Reuters/the Defense Ministry/Yonhap)

Wanajeshi wa Korea Kusini wapiga doria eneo la mpakani, DMZ, kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini

Alisema miaka 20 ya diplomasia na juhudi nyenginezo imeshindwa kuishawishi serikali hiyo ya kikyomunisti kusitisha uendelezaji wa mpango wake wa nyuklia, jambo ambalo Tillerson alilitaja kama kitisho kinachoongezeka kila mara.

Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini Yun Byung-se aliwaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake na Marekani zina lengo moja la kuhakikisha kwamba wanamaliza zana za nyuklia za Korea Kaskazini.

Rais Trump wa Marekani anatafakari kutumia mbinu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini

Yun pia amesema mpango wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ambao Korea Kusini inautumia unalenga tu kujilinda dhidi ya Korea Kaskazini na wala sio nchi nyengine, kwani China inasema mpango huo unahujumu usalama wake.

Rais Donald Trump anaonekana kutafakari kutumia mbinu zote zikiwepo za kijeshi, ili kusitisha mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini kabla taifa hilo, halijakuwa na uwezo wa kuunda silaha yenye uwezo wa kufika Marekani.

Marekani inaiona China kama nchi muhimu kwa sana iwapo inataka ufanisi wa aina yoyote ile katika kuishawishi Korea Kaskazini, ibadilishe mwenendo wake katika masuala ya Nyuklia, kwani China ndio rafiki wa pekee wa karibu wa Korea Kaskazini mwenye uwezo mkubwa.

Korea Kaskazini imeongeza kasi katika juhudi zake za kuunda silaha za nyuklia, jambo linalokiuka maazimio kadhaa ya Umoja wa Mataifa na taifa hilo linaonekana kutobabaishwa na vikwazo vikali inavyowekewa na jamii ya kimataifa.

Mwandishi: Jacob Safari/AP/DPA/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com