1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Uvamizi wa Israel wazusha wasiwasi wa kimataifa

Bruce Amani
15 Novemba 2023

Operesheni ya jeshi la Israel katika hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, inayolenga kile inachosema ni kituo cha kamandi ya Hamas kilicho kwenye mahandaki ya chini ya hospitali hiyo, imezusha wimbi la shutuma za kimataifa.

https://p.dw.com/p/4Yqy1
Mji wa Gaza | Muuguzi wa hospitali ya Al-Ahli
Moja ya muuguzi katika hositali ya Al Ahli akimhudumia mtoto aliyejeruhiwa kutokana na makombora yanayorushwa na Israel GazaPicha: Montaser Alswaf/Anadolu/picture alliance

Jeshi lilitangaza kuwa linafanya operesheni ya sahihi na inayowalenga Hamas katika eneo maalum la hospitali hiyo ambako Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kuna karibu watu 2,300 wakiwemo wagonjwa, wahudumu na Wapalestina waliopoteza makazi.

Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundu wameelezea hofu na kuwataka watu hao walindwe.

Marekani yasema Hamas walitumia hospitali kutekeleza operesheni

Mkuu wa masuala ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema amekasirishwa na ripoti za uvamizi huo uliofanywa na jeshi la Israel akisema hospitali sio viwanja vya mapambano na kwa hiyo lazima operesheni hiyo ya umwagaji damu isitishwe mara moja.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hakuna sehemu yoyote ya Gaza ambayo askari wake hawatofika. Wakati huo huo, Israel imesema itaruhusu malori yaliyobeba msaada unaopelekwa Ukanda wa Gaza kujaza mafuta.

Hii ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita hivyo ambapo Israel imeruhusu kuingizwa mafuta Gaza.