Uturuki yaitaka Marekani kuvunja uhusiano na YPG | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Turkey

Uturuki yaitaka Marekani kuvunja uhusiano na YPG

Waziri mkuu wa Uturuki amesema anatarajia serikali mpya ya Marekani kusitisha ugavi wa silaha kwa kundi la wanamgambo wa Kikurdi YPG nchini Syria na kuwa uongozi wa rais Obama ulihusika katika usambazaji huo wa silaha.

Katika taarifa aliyoisoma bungeni kwa wabunge wa chama tawala cha AKP, waziri mkuu Binali Yildirim alisema kuwa Marekani haipaswi kuruhusu ushirikiano wake na Uturuki kutatizwa na kundi la kigaidi.
Uturuki imekasirishwa na hatua ya Marekani ya kuunga mkono kundi hilo la wanamgambo la YPG ambalo limeibuka kama mshirika mkuu wa Marekani katika kukabiliana na kundi la kigaidi linalojiita dolala kiislamu nchini Syria.
Wakati huo huo, serikali ya Uturuki inanuia kuongeza muda wa hali ya tahadhari iliyowekwa kufuatia jaribio la kuipindua serikali kati kati ya mwezi Julai mwaka uliopita. Yildrim aliwaambia wabunge hao kuwa hoja ya kuongeza muda huo kwa siku 90 kutoka Januari 19 itawasilishwa bungeni wiki hii.

 Rais Reccep Tayyip Erdogan alitoa tangazo la hali ya hatari baada ya jaribio la kuipindua serikali yake mnamo Julai15 lililolaumiwa kwa mhubiri mwenye makao yake Marekani Fet-hullah Gulen. Jaribio hilo lilipelekea msako mkubwa dhidi ya wapinzani wa serikali katika sekta nyingi ikiwa ni pamoja na polisi na jeshi.

Msako waimarishwa dhidi ya mshukiwa

Na huku msako ukiendelezwa dhidi ya mshambuliaji wa kilabu kimoja mjini Istanbul mkesha wa mwaka mpya, shirika la habari la Dogan liliripoti kuwa, maafisa wa serikali nchini humo, leo wamewazuilia raia wawili wa kigeni katika uwanja mkuu wa ndege wa Istanbul wakishukiwa kuhusika katika shambulizi hilo dhidi ya kilabu cha Reina, lililodaiwa kutekelezwa na kundi la wanamgabo la dola la kiislamu na kusababisha vifo vya watu 39.

Istanbul Reina nightclub nach Anschlag (Getty Images/AFP/O. Kose)

Kilabu cha Reina kilichoshambuliwa mkesha wa mwaka mpya

Wawili hao walikamatwa walipokuwa wakiingia katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ataturk na wamepelekwa katika makao makuu ya polisi ya Istanbul kuhojiwa.
Wakati huo huo, gazeti la Hurriyet limesema kuwa mwanamke mmoja alietambuliwa na vyombo vya habari nchini Uturuki kuwa mke wa mshukiwa huo wa shambulizi la kigaidi dhidi ya kilabu cha Reina huko Istanbul, aliwaambia maafisa wa polisi kuwa hakufahamu kuwa mumewe ni mwanachama wa kundi hilo la dola la kiislamu.
Kundi hilo limedai kuhusika katika shambulizi hilo huku polisi wakiendelea kumsaka msahmbuliaji huyo.
Mwanamke huyo alizuiliwa katika mji wa Kati wa Konya kama sehemu ya uchunguzi. Wote mke na mume hawajatambuliwa kwa majina.
Gazeti hilo la Hurriyet limeripoti kuwa mwanamke huyo alisema kuwa alifahamu kuhusu shambulizi hilo kupitia runinga na kuwaambia polisi kuwa hakufahamu kuwa mume wake alikuwa mwanachama wa kundi la kigaidi.


Mwandishi: Tatu Karema/ APE/ DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com