Uturuki kujiunga na operesheni dhidi ya IS | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uturuki kujiunga na operesheni dhidi ya IS

Bunge la Uturuki linatarajiwa kuupigia kura muswaada utakaotoa mamlaka kwa serikali mpya kufanya uvamizi wa kijeshi nchini Syria na Iraq. Hayo yanajiri wakati mashambulizi yakiendelea katika moaka wa Syria na Iraq

na kuyakubalia majeshi ya kigeni kutumia mipaka yake katika uwezekano wa kufanya mashambulizi dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu. Lakini nchi hiyo bado haijafafanua wazi ni jukumu gani ambalo linatarajiwa kutekelezwa na Uturuki katika operesheni inayoongozwa na Marekani dhidi ya wanamgambo hao wenye itikadi kali.

Serikali ya Uturuki haieleweki kuhusu namna inavyolenga kushirikiana katika operesheni ya mashambulizi ya muungano inayoongozwa na Marekani dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu - IS, au ni umbali gani inatarajiwa kupambana na kundi hilo lenye itikadi kali za kiislamu, lakini muswaada huo unaweka msingi wa kisheria.

Marekani ina kambi kubwa ya jeshi la angani katika eneo la Incirlik, nje ya mji wa Adana nchini Uturuki, ijapokuwa mashambulizi yake nchini Iraq na Syria kufikia sasa yametokea katika manowari za kambi zao za kijeshi katika mataifa ya Kiarabu.

Syrien - Kurden in Kobane

Wapiganaji wa Kikurdi wanapambana na wanamgambo wa IS katika mji wa mpakani wa Kobane

Bunge la Uturuki katika miaka ya nyuma liliidhinisha operesheni za kulituma jeshi lake nchini Iraq na Syria ili kuwashambulia wanamgambo wa Kikurdi waliopigania kujitenga au kuzuia vitisho kutoka utawala wa Syria, lakini muswaada wa leo unayapanua mamlaka hayo ili kuangazia vitisho vya wanamgambo wa IS ambao wanadhibiti sehemu kubwa la mpakani nchini Iraq na Syria, na katika maeneo mengine hadi katika mipaka ya nchi hizo na Uturuki.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa wito wa kuundwa ukanda uliozuiliwa ndani ya Syria pamoja na kutangaza amri ya kutoruka ndege ili kuilinda mipaka ya Uturuki na kuzuia uhamiaji wa wakimbizi. Pia ametoa wito wa kupewa mafunzo na silaha, upinzani unaopambana na utawala wa Rais wa Syria Bashar al Assad.

Na wakati hayo yakiendelea bungeni, wapiganaji wa IS wameikaribia milango ya mji mmoja muhimu wa Kikurdi katika mpaka wa Syria na Uturuki. Wapiganaji wa Kikurdi wakisaidiwa na mashambulizi ya kutokea angani yanayoongozwa na Marekani wanaendelea kupambana vikali ili kuuzuia mji wa Kobane kuanguka mikononi mwa wapiganaji wa IS.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria limeonya kuwa kuna hofu kubwa kuwa kundi la IS huenda likafanikiwa kuingia katika mji wa Kobane hivi karibuni. Mapigano hayo yamejiri wakati milipuko mikubwa ikiutikisa mji mkuu wa Iraq, Baghdad pamoja na mji wa tatu kwa ukubwa nchini Syria, Homs, ambapo watoto 41 ni miongoni mwa waliouawa mjini Homs. Tayari muungano unaoongozwa na Marekani umefanya karibu mashambulizi saba katika ngome za IS kariobu na mji wa Kobane katika kipindi cha siku tano hadi kufikia jana.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com