1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMashariki ya Kati

Utulivu warejea kwenye mpaka wa Israel na Ukingo wa Gaza

3 Mei 2023

Hali ya utulivu imerejea kwenye mpaka wa Israel na Ukanda wa Gaza baada ya pande hizo mbili kuafikiana kusitisha mapigano yaliyohusisha maroketi na hujuma za ndege za kivita.

https://p.dw.com/p/4QprI
Mfumo wa kujilinda na makombora wa Israel
Mfumo wa kujilinda na makombora wa Israel Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Mapambano hayo ya tangu jana mchana yalichochewa na kifo cha Mpalestina aliyekuwa kwenye mgomo wa kula akiwa katika jela nchini Israel. 

Tangazo la kusitishwa mapigano lilitolewa mapema leo Jumatano na kundi la wanamgambo wa kipalestina liitwalo Islamic Jihad, ambalo lilivurumisha makombora kuelekea Israel tangu jana baada ya kutangazwa kifo cha Khader Adnan, Mpalestina aliyeaga dunia akiwa katika jela nchini Israel.

Jeshi la Israel lilijibu mashambulizi hayo ya maroketi kwa kufanya hujuma kwenye Ukanda wa Gaza kwa kutumia ndege za kivita. Upande wa Wapalestina umesema mtu mmoja ameuwawa na wengine zaidi ya watano wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo ya Israel.

Khader Adnan
Khader Adnan Picha: Mohamad Torokman/REUTERS

Wapatanishi kutoka mataifa ya Qatar, Misri na Umoja wa Mataifa walifanya juhudi kutwa nzima jana kutafuta makubaliano ya kusitisha uhasama, na mnamo Alfajiri ya leo hali ya utulivu ilirejea baada ya wanamgambo wa Kipalestina kusitisha ufyetuaji maroketi.

Israel yasema hakuna roketi lilirotushwa kutokea Gaza tangu Alfajiri ya Jumatano 

Israel nayo imetangaza mchana huu kurejea kwa "hali yakawaida" kwenye mpaka wake na Ukanda wa Gaza. Jeshi la nchi hiyo limearifu hapakuwa na maroketi yaliyorushwa kutokea Gaza tangu majira ya Alfajiri.

Hadi jana jioni wanamgambo wa kipalestina walikuwa wamefyetua kiasi maroketi 100 kuelekea upande wa kusini mwa Israel. Israel ilijibu kwa kuyashambulia kile imeyataja kuwa vituo vya kijeshi vya makundi ya wapiganaji wa kipalestina pamoja mahandaki.

Kifo cha Mpalestina Khader Adnan katika gereza nchini Israel kimezusha ghadhabu kubwa miongoni mwa jamii ya Wapalestina huko Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Adnan aliyekuwa na umri wa miaka 45 na anayetokea mji wa Jenin ulio eneo la Ukingo wa Magharibi alifariki dunia siku ya Jumanne baada ya kufanya mgomo wa kula kwa siku 87.

Alikuwa akipinga kukamatwa kwake na vikosi vya Israel vilivyomtuhumu kuwa na mahusiano na kundi la wanamgambo la Islamic Jihad.

Wapalestina waomboleza kifo cha Adnan kama shujaa 

Familia ya Khader Adnan
Familia ya Khader Adnan Picha: Raneen Sawafta/REUTERS

Kifo chake kutokana na mgomo wa kula kimemfanya kuwa shujaa kwa upande wa Wapalestina. Aina hiyo ya mgomo imekuwa ikutumiwa na wapalestina kadhaa kuonesha upinzani wa kushikiliwa kwenye jela nchini Israel bila kufunguliwa mashtaka.

Hata hivyo kifo cha Adnan ni cha kwanza kutokea katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Mamia ya wapalestina waliteremka mitaani hapo jana kuomboleza kifo cha Adnan, ambacho viongozi wa Palestina wamekianisha kuwa mauaji ya kupangwa. 

Wakili wake na daktari kutoka shirika moja la Haki za Binadamu waliomtembelea Adnan hivi karibuni walizituhumu mamlaka za Israel kwa kutompatia mfungwa huyo huduma ya matibabu.

Kiongozi wa kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza, Ismail Haniyeh amezitaka mamlaka za Israel kurejesha mwili wa Adnan kwa familia yake. Kundi la Islamic Jihad nalo limesema ingawa makabiliano na Israel yamesitishwa lakini safari ya kuipinga dola hiyo ya kiyahudi bado inaendelea.