1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNRWA kusitisha huduma zake Gaza kutokana na uhaba wa mafuta

Sylvia Mwehozi
14 Novemba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, limeonya kwamba bohari yake ya mafuta katika Ukanda wa Gaza, imekauka na huenda wakalazimika kusimamisha shughuli zake ndani ya saa 48.

https://p.dw.com/p/4Ym1t
Gaza Hamas Israel Vita vya Mashariki ya Kati; Kambi ya wakimbizi ya Jabalia
Mwonekano wa shimo lililojitokea nyuma ya shule ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) inayotumika kama makazi ya Wapalestina waliokimbia makazi yao, baada ya mashambulizi ya anga ya Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia huko Gaza City, Gaza mnamo Novemba 12, 2023.Picha: Fadi Alwhidi/Andalou/picture alliance

Mkuu wa shirika hilo Thomas White aliandika kupitia ukurasa wa X kwamba UNRWA, imekuwa ikitumia mafuta kutoka katika hifadhi yake, lakini nako mafuta yamewaishia. Afisa huyo amesema hakuna mafuta yaliyoruhusiwa kuingia Gaza tangu Oktoba 7, wakati Hamas walipofanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Israel.

Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas pia ilisema mapema siku ya Jumatatu kwamba hospitali zote kaskazini mwa Gaza hazifanyi kazi tena kutokana na uhaba wa mafuta.

Soma pia: UN yawakumbuka watumishi wake waliouawa kwenye vita vya Mashariki ya Kati

Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani Joe Biden ametoa wito kwa Israel wa kuilinda hospitali kubwa ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza. Biden ametoa wito huo wakati shirika la afya ulimwenguni WHO likisema hospitali hiyo haifanyi kazi tena. 

Wafanyakazi katika hospitali hiyo wamedai kuzingirwa, baada ya kituo hicho kushambuliwa mara kadhaa kwa mabomu. Wamesema Israel inawapiga risasi watu wanaotoka nje ya jengo hilo. Madai hayo yamekanushwa na Israel inayodai kwamba wanamgambo wa Hamas wanatumia mtandao wa mahandaki ulio chini ya hospitali.