1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

UNHCR: Wakazi wa Gaza hawapaswi kuvuka kuingia Misri

Tatu Karema
12 Aprili 2024

Mkuu wa shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Filipo Grandi, amesema matarajio ya wakazi wa Gaza kuvuka kuingia Misri huenda yakatatiza utatuzi wa mzozo kati ya Israel na Palestina

https://p.dw.com/p/4ehrX
Mkuu wa shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Matiafa, UNHCR, Filipo Grandi,
Mkuu wa shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Matiafa, UNHCR, Filipo Grandi,Picha: Jean-Guy Python/AFP-Pool/KEYSTONE/dpa/picture alliance

Grandi ameliambia shirika la habari la Reuters mjini Geneva nchini Uswisi kwamba lazima watumie njia zote kuepusha kuondoka kwa wakazi hao wa Gaza kutoka eneo hilo.

Mkuu huyo wa UNHCR ameongeza kuwa hatua hiyo itasababisha mzozo mwingine wa wakimbizi kutoka Gaza kuingia Misri na kwamba hali hiyo haikubaliki na wajibu wa kuiepuka uko mikononi mwa Israel.

Soma pia:Raia wengi wa Gaza wanakimbilia eneo la mpakani na Misri wakihofia mapigano kati ya Israel na Hamas

Grandi ameongeza kuwa UNHCR inahifadhi mahema na bidhaa nyingine na kushirikiana na mataifa katika kanda hiyo juu ya mipango ya dharura ya uwezekano wa kuwasili kwa wakimbizi kutoka Gaza.

Wafanyakazi wa msaada Gaza walalamikia ukosefu wa vifaa vya mawasiliano

Wafanyakazi wa msaada katika Ukanda wa Gaza wamesema kuwa hawana vifaa vya mawasiliano ndani ya eneo hilo kufanya kazi vizuri. Mratibu wa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo Jamie McGoldrick amesema hali hiyo inawaweka wafanyakazi hao kwenye hatari.

Soma pia:Marekani yashirikiana na washirika kuanzisha njia mpya za misaada kuingia Gaza

McGoldrick ameongeza kuwa Israel inaamini kuwa jukumu lake linakamilika wakati wanaingiza malori ya misaada  kutoka eneo la mpaka wa israel la Kerem Shalom kuingia katika eneo hilo la Palestina na kusema hivyo sivyo inavyopaswa kuwa.

Ufaransa yawaonya raia wake kutosafiri katika baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati

Wakati mazungumzo yanayolenga kusitisha vita vilivyodumu kwa miezi sita kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas yakiendelea, hofu kwamba Iran inaweza kufanya mashambulizi hivi karibuni dhidi ya Israel, imeichochea Ufaransa kuwaonya raia wake kutosafiri nchini humo, Lebanon, Israel na Mamlaka ya Palestina katika siku zijazo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akizungumza wakati wa kongamano la kiuchumi la Brazil na Ufaransa
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: ISAAC FONTANA/EPA/picture alliance

Hatua hii inakuja baada ya ubalozi wa Marekani nchini Israel kutangaza kwamba inadhibiti safari za wanadiplomasia wake kutokana na hofu ya usalama.

Mvutano kati ya Iran na Israel unaongezeka, waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant leo amesema kwamba Israel na mshirika wake Marekani ziko bega kwa bega kukabiliana na kitisho  cha Iran.

Soma pia: Israel yasema imejitayarisha kupambana na shambulizi lolote kutoka Iran

Gallant ametowa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na kiongozi wa kamandi kuu ya kijeshi ya Marekani Michael Kurilla. Lakini kwa upande mwingine taarifa iliyotolewa leo na Ikulu ya Marekani na msemaji wa baraza la usalama la Marekani, John Kirby,  inasema kitisho cha Iran dhidi ya Israel kiko wazi na huenda kikatekelezwa kwa uhakika.

Miito yatolewa kwa Iran kutoishambilia Gaza

Wakati Ufaransa, ikiwashauri raia wake wajizuie kusafiri katika nchi kadhaa za Mashariki ya kati pamoja na Iran, Urusi na Ujerumani zimeitaka Iran kutofanya mashambulizi dhidi ya Israel.

Iran imetishia kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi baada ya shambulizi la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo mjini Damascus nchini Syria mnamo Aprili 1.