UN Climate change Summit | Masuala ya Jamii | DW | 23.09.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

UN Climate change Summit

China na Japan zatangaza kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira

default

Waziri Mkuu wa Japan, Yukio Hatoyama akizungumza kwenye mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa, New York, Marekani.

Rais wa China Hu Jintao amesema nchi yake iko tayari kupunguza kwa kiwango kikubwa utoaji wa gesi zinazochafua mazingira ifikapo mwaka 2020, huku Rais Barack Obama wa Marekani kwa upande wake akiyataka mataifa yote kufanya jitihada za kukabiliana na ongezeko la ujoto duniani.

Rais Hu Jintao alitoa ahadi hiyo kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa uliohudhuriwa na viongozi wa nchi na serikali kutoka duniani kote. Rais Hu Jintao ameongeza shinikizo kwa mataifa yaliyoendelea kabla ya mazungumzo ya hali ya hewa yatakayofanyika mwezi Desemba, mwaka huu mjini Copenhagen, Denmark.

Kiongozi huyo wa China, hata hivyo, ameambatanisha suala la ustawi wa uchumi wa nchi yake na utekelezaji wa ahadi hiyo.

Kwa upande wa Rais Obama, alizungumzia kazi inayofanywa na utawala wake katika mabadiliko ya hali ya hewa tangu alipochukua madaraka mwezi Januari, mwaka huu na kusema kuwa Marekani imejitoa kwa dhati kuchukua hatua. Hata hivyo, Rais Obama hakutoa mapendekezo mapya na hakulitaka baraza la Senate kupitisha haraka muswada wa hali ya hewa, jambo ambalo waangalizi wengi wanaliona kuwa ni muhimu katika kufikiwa mkataba wa kimataifa. Zaidi Rais Obama anasema:

''Najisikia fahari kusema kuwa Marekani imefanya mengi katika hatua za kuleta ufahamu juu ya nishati zisizochafua mazingira na kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira katika miezi minane iliyopita kuliko wakati mwingine wowote katika historia.''

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Japan, Yukio Hatoyama amepongezwa kwa ahadi yake ya kutoa msaada kwa nchi zinazoendelea katika mpango wa mabadiliko ya hali ya hewa na kurudia lengo lake kwa Japan kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira kwa asilimia 25, kutoka mwaka 1990 ifikapo mwaka 2020. Hatoyama anasema:

''Kwa lengo la kipindi cha hivi sasa, Japan itatenga kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2020 ikilinganishwa na kiwango cha mwaka 1990 ili kuweza kuzuia kupanda kwa hali ya joto duniani.''

Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki-Moon, alisisitiza ulazima wa kutoa ishara ya nia nzuri kama msingi wa kuleta mafanikio kwenye mkutano wa baadaye utakaofanyika mjini Copenhagen. Wajumbe watakaohudhuria kwenye mkutano huo watajadili mkataba mpya wa kimataifa kuhusu ulinzi wa hali ya hewa utakaochukua nafasi mkataba wa sasa wa Kyoto, ambao awamu yake ya kwanza inamalizika mwishoni mwa mwaka 2012. Aidha, Bwana Ban amesema kupitishwa mkataba huo mpya kutakuwa na maana ya kuleta neema, usalama na haki zaidi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman.

 • Tarehe 23.09.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Jmy7
 • Tarehe 23.09.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Jmy7

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com