1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wapendekeza kuimarishwa sera ya uhamiaji

16 Mei 2024

Mataifa 15 ya Umoja wa Ulaya yametaka kuimarishwa zaidi kwa sera ya kusimamia suala la kupokea waomba hifadhi na kurahisisha mchakato wa kuwahamisha wahamiaji wasiokuwa na vibali hadi nchi maskini.

https://p.dw.com/p/4fwq2
Wahamiaji kutoka Syria huko Cyprus
Wahamiaji kutoka Syria huko CyprusPicha: Petros Karadjias/picture alliance/AP

Mataifa 15 ya Umoja wa Ulaya yametaka kuimarishwa zaidi kwa sera ya kusimamia suala la kupokea waomba hifadhi na kurahisisha mchakato wa kuwahamisha wahamiaji wasiokuwa na vibali hadi nchi maskini, ikiwa ni pamoja na waliookolea kutoka baharini.

Mapendekezo  hayo, yaliyoandikwa kwenye  barua  iliyokabidhiwa halmashauri ya Umoja wa  Ulaya yanajiri chini ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya, ambapo vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vinavyopinga uhamiaji vinatarajia kupata mafanikio.

Soma: Bunge la EU lapitisha mageuzi makubwa ya sera ya wahamiaji

Barua hiyo inaitaka Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ambayo ni taasisi ya maamuzi ya mwisho, kupendekeza njia mpya na suluhu za kuzuia wahamiaji kuingia Ulaya.

Mataifa hayo ni pamoja na Italia na Ugiriki ambayo yanapokea idadi kubwa ya watu wanaofanya safari ya hatari kuvuka Bahari ya Mediterania kuingia Ulaya wengi wakitafuta kuepuka umaskini, vita au mateso, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.

Aidha mataifa hayo yanahoji kwamba inapaswa kuwa rahisi kuwatuma waomba hifadhi kwa nchi maskini wakati maombi yao ya ulinzi yakitathminiwa.