1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waunda chombo kusimamia albino

Caro Robi27 Machi 2015

Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa hapo limeamua kumteua mtaalamu wa kuchunguza maovu wanayotendewa watu wenye ulemavu wa ngozi ambao wamekuwa wakizidi kushambuliwa Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/1EyKM
Watoto wenye ulemavu wa ngozi katika Skuli ya Msingi ya Mitndo, Tanzania.
Watoto wenye ulemavu wa ngozi katika Skuli ya Msingi ya Mitndo, Tanzania.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Baraza hilo la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 47 lilipitisha azimio kwa kauli moja la kuundwa wadhifa wa mtaalamu wa kuchunguza maovu dhidi ya Albino ambaye atahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.

Baraza hilo limeeelezea wasiwasi mkubwa kutokana na mashambulizi na mauaji ya kikatili dhidi ya Albino wakiwemo wanawake, watoto, walemavu na wazee.

Azimio hilo liliwasilishwa na Algeria kwa niaba ya kundi la mataifa ya bara la Afrika baada ya Mkuu wa Kamisheni ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein mapema mwezi huu kulaani vikali mashambulizi dhidi ya watu hao wenye ulemavu wa ngozi ambayo alisema yameongezeka katika nchi za kanda ya Afrika Mashariki.

Watu 15 wauawa ndani ya nusu mwaka

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kiasi cha watu 15 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa nchini Tanzania, Malawi na Burundi na albino wengine wametekwa nyara, kujeruhiwa kwa kakatwa viungo vya mwili na wengine wamelazimika kuyatoroka makaazi yao kuepuka ukatili huo.

Mama mwenye ulemavu wa ngozi Leondiah na binti yake nchini Kenya.
Mama mwenye ulemavu wa ngozi Leondiah na binti yake nchini Kenya.Picha: DW/G. Ketels

Mashambulizi dhidi ya Albino huwa mara nyingi yanachochewa na imani za kishirikina kutokana na dhana potofu kuwa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi husaidia waganga na wachawi kufanya matambiko yanayoleta utajiri na ufanisi.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya Albino hasa nchini Tanzania katika kipindi cha hivi karibuni huenda kukahususishwa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo baadhi ya wanasiasa wanatafuta nguvu za kishirikina kujipatia ushindi katika uchaguzi huo.

Tanzania yapiga marufuku uganga

Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku shughuli za kiganga nchini humo mwezi Januari kama sehemu ya hatua inazozichukua kukomesha ukatili dhidi ya Albino.

James, mlemavu wa ngozi nchini Tanzania.
James, mlemavu wa ngozi nchini Tanzania.Picha: picture-alliance/CTK/T. Junek

Kati ya watu 1,400 nchini humo ni Albino ikilinganishwa na takwimu zilizoko katika nchi za magharibi ambapo kati ya watu 20,000 mmoja ndiye Albino. Azimio hilo lililopitishwa hapo jana pia limeelezea wasiwasi wake kuwa katika baadhi ya sehemu duniani watu wenye ulemavu wa ngozi wanakabiliwa na unyanyapaa katika jamii na wanazuiwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo na kukabiliwa na vitendo vya ukiukaji wa haki zao za binadamu.

Umoja wa Mataifa umesema juhudi zaidi zinahitajika ili kuweza kushughulikia changamoto wanazokabiliana nazo Albino na mtaalamu huyo atakayeteuliwa na Rais wa baraza hilo la umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamu atakuwa na jukumu la kuripoti visa vya ukatili dhidi ya albino, kusaidia katika kufutilia mbali dhana potofu, unyanyapaa na mila zilizopitwa na wakati kuwahusu Albino.

Mwandishi: Caro Robi/AFP
Mhariri: Mohamed Abdulrahman